Na. Veronica E. Mwafisi-Dar-es-Salaam
Tarehe 02 Machi, 2022
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi
amesema, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa kupokea, kufuatilia na kushughulikia
malalamiko (e-Mrejesho) kumekuwa na mwitikio chanya wa wananchi na watumishi wa
umma kuutumia mfumo huo, ambao umeiwezesha Serikali kupokea na kushughulikia
kwa wakati jumla ya maoni na malalamiko 239,196 yaliyowasilishwa katika Taasisi
za Umma.
Bw. Daudi amesema hayo
jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa
mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na
pongezi (e-Mrejesho) kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa Sekretarieti za Mikoa,
Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Wakala na Idara Zinazojitegemea ambao
wamepewa dhamana ya kushughulikia malalamiko kwenye taasisi zilizopo Kanda ya Mashariki.
Bw. Daudi amesema kuwa, miaka
ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo wa kielektroniki haikuwa rahisi kushughulikia
malalamiko kwa wakati na kuwa na takwimu halisi za maoni na malalamiko
yaliyofanyiwa kazi ambazo zinatumiwa na Serikali kama mrejesho wa kuboresha
huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma kwa wananchi.
Aidha, Bw. Daudi
ameeleza kuwa, Ofisi ya Rais – UTUMISHI kupitia Idara ya Ukuzaji Maadili
imejipanga kuendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA katika
taasisi zote za umma nchini, ili kuwajengea uwezo wa kutumia vema mfumo huo wa
kieletroniki kushughulikia malalamiko yote yanayowasilishwa na wananchi na
wadau kwa wakati.
Bw. Daudi ameongeza
kuwa, Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa kwa namna ambayo inaongeza uwazi,
uwajibikaji na usikivu kwa watendaji Serikalini, kwani mfumo unawawezesha viongozi
katika ngazi mbalimbali kuona na kufuatilia namna ambavyo malalamiko au maoni
yanavyoshughulikiwa.
“Endapo kutakuwa na
ucheleweshwaji wa kutoa mrejesho au uzembe wa aina yoyote, mfumo unampa fursa kiongozi
katika taasisi husika kuchukua hatua stahiki kwa wakati,” Bw. Daudi amefafanua.
Sanjari na hilo, Bw.
Daudi amesema kuwa, mfumo huo ni rahisi kuutumia kwa kuwa unamuwezesha mtumishi
na mwananchi wakati wote na popote alipo kutuma maoni au malalamiko na kupokea
mrejesho kupitia tovuti au simu za kiganjani.
Akisisitiza suala la
uwajibikaji, Bw. Daudi ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo, kuhakikisha
wanaratibu ushughulikiaji wa malalamiko kwa wakati ili mfumo huo uwe na tija
kwa wananchi na manufaa kwa Serikali katika kuboresha huduma inazozitoa kwa
wananchi.
Akitoa neno la
utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu kuzungumza na washiriki wa
mafunzo hayo, Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais – UTUMISHI,
Bi. Leila Mavika amesema kuwa, njia ambazo zilikuwa zikitumika kuwasilisha
malalamiko hapo awali zilisababisha changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosekana
kwa takwimu sahihi za utunzaji wa takwimu za malalamiko ambazo hutumiwa na
Serikali kuboresha huduma na kufanya maamuzi.
Bi. Mavika ameeleza
kuwa, kabla ya Serikali kuanzisha mfumo wa kushughulikia malalamiko
kielektroniki, wananchi hawakuwa na fursa ya kupata mrejesho wa malalamiko yao
kwa wakati hivyo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) iliona ni vema kuandaa
mfumo wa kielektroniki ambao kwa kiasi kikubwa utaongeza uwajibikaji katika
eneo la kushughulikia malalamiko.
Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara yake ya Ukuzaji
wa Maadili na Idara ya Mifumo ya TEHAMA inatoa mafunzo ya kutumia mfumo wa
e-Mrejesho kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA katika Taasisi za Umma ziliozopo mikoa
ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, yanayofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku
nne (4) katika Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na Maafisa Malalamiko
na TEHAMA wa Taasisi za Umma ziliozopo mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara,
kabla ya kufungua mafunzo ya kuutumia mfumo wa e-Mrejesho kwa maafisa hao
yanayofanyika jijini Dar es Salaam katika
Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Bi. Leila
Mavika akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais- UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi kufungua mafunzo ya
matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko,
mapendekezo, na maulizo (e-Mrejesho) kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa
Taasisi za Umma ziliozopo mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara yanayofanyika
jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
Mwenyekiti wa mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa
mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, na maulizo
(e-Mrejesho), Bw. Selemani Majindo akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi mara baada ya Naibu
Katibu Mkuu huyo kufungua mafunzo ya kutumia mfumo wa e-Mrejesho kwa Maafisa
Malalamiko na TEHAMA wa Taasisi za Umma ziliozopo mikoa ya Dar es Salaam, Lindi
na Mtwara yanayofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na
kufuatilia malalamiko, mapendekezo, na maulizo (e-Mrejesho) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala
Bora, Bw. Xavier Daudi wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dar
es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa Taasisi za Umma
ziliozopo mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, mara baada ya kufungua
mafunzo ya kuutumia mfumo wa e-Mrejesho kwa maafisa hao yanayofanyika jijini
Dar es Salaam katika
Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akiwa katika picha ya pamoja na na baadhi ya
viongozi wa ofisi yake pamoja na wawezeshaji wa mafunzo ya kutumia mfumo wa
e-Mrejesho kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa Taasisi
za Umma ziliozopo mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, mara baada ya
kufungua mafunzo kwa maafisa hao yanayofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Kodi.
No comments:
Post a Comment