Na. Veronica Mwafisi-Makete
Tarehe 21 Machi, 2022
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), Mhe. Dennis Londo ameupongeza
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kujenga bweni la wanafunzi wa kike
katika Shule ya Sekondari Mang’oto wilayani Makete kwa lengo la kuwaondolea changamoto
ya kutembea umbali mrefu wanafunzi hao, hivyo kuwawezesha kupata muda wa
kutosha wa kuzingatia masomo yao.
Mhe. Londo amesema kuwa, jitihada za
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ukiwemo
wa ujenzi wa bweni hilo la wanafunzi wa kike katika
Shule ya Sekondari Mang’oto, ni kielelezo cha namna Serikali ya
Awamu ya Sita inavyozingatia mahitaji ya wananchi wake katika maeneo yenye
uhitaji.
Mhe. Londo ameongeza kuwa, wananchi
wanapaswa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan aliyedhihirisha nia yake ya dhati kwa vitendo katika kumkomboa
mtoto wa kike kupitia TASAF.
Mhe. Londo amesema, kamati yake inaunga
mkono jitihada hizo za TASAF katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii
inayowanufaisha wananchi katika sekta muhimu hususani nguvu kubwa ya kuboresha mazingira
ya elimu kwa Mtanzania.
Sanjali na hilo, Mhe. Londo
amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa
bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Mang’oto, ambapo nguvu
kazi yao imekuwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Makete, Bw. William Makufwe amesema, kitendo cha Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufadhili ujenzi wa bweni la shule ya wasichana
Mang’oto kimesaidia watoto wa kike kupaka elimu bora kwa manufaa yao na yenye
tija kwa maendeleo ya taifa.
“Mhe. Mwenyekiti, bweni hili limejengwa
ili kusaidia watoto wa kike, kwani kata hii ya Mang’oto ina milima na mabonde hivyo
inakuwa ni ngumu kwa wanafunzi wa kike kutoka katika makazi yao na kufika
shuleni kwa wakati, na ndio maana tuliomba TASAF watusaidie kujenga mazingira
bora ya kuwapatia elimu wanafunzi wa kike ambao sasa watalala katika bweni hili
na kuzingatia vizuri masomo yao,” Bw. Makufwe amefafanua.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Ladislaus Mwamanga amesema Kamati ya Kudumu ya
Bunge imeridhishwa na utekelezaji mzuri wa miradi ya TASAF inayozingatia
viwango vya juu kulingana na thamani ya fedha.
Bw. Mwamanga amesema utekelezaji huo
mzuri wa miradi ya TASAF unatokana na ushirikiano mzuri walionao Kamati ya
USEMI, ambayo imekuwa ikitoa ushauri mzuri uliosaidia TASAF kutekeleza vizuri
miradi yake.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa (USEMI) imekamilisha ziara yake ya kikazi ya kukagua
utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmshauri ya Wilaya Mji Njombe pamoja na
Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah
Chaurembo akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ilindiwe mara baada ya kukagua
bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Mang’oto lillojengwa kwa
ufadhili wa TASAF, wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua
utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya Makete.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakisikiliza taarifa ya
Maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa bweni la shule ya Sekondari Mang’oto wakati wa
ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Watatu kutoka kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Ladislaus Mwamanga.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), Mhe. Dennis Londo akizungumza na wajumbe
wa Kamati hiyo pamoja na wananchi wa Kijiji cha Ilindiwe mara baada ya kukagua
mradi wa ujenzi wa bweni la
wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Mang’oto, wakati wa ziara ya kikazi
ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika
Halmashauri ya Wilaya Makete.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na wananchi wa Kijiji cha Ilindiwe
wakitoka kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la
wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Mang’oto, wakati wa ziara ya kikazi
ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika
Halmashauri ya Wilaya Makete.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mang’oto wakiimba wimbo maalum wa
kuwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa, wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji
wa Miradi ya TASAF
katika Halmashauri ya Wilaya Makete.
No comments:
Post a Comment