Na.
James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 16 Machi, 2022
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha mwaka mmoja cha
uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kuzingatia maslahi ya Watumishi
wa Umma hivyo kujenga morali ya kiutendaji kwa watumishi hao.
Mhe. Jenista
amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari
uliolenga kuuhabarisha umma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita
katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Jenista
amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imesimamia mageuzi makubwa kwenye Utumishi wa Umma katika kutazama
maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji madaraja ambapo imewapandisha madaraja Watumishi wa Umma 190,781 wenye sifa
stahiki na katika zoezi hilo jumla ya shilingi bilioni 39,649,988, 204
zimetumika.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa Serikali imelipa madeni ya
mishahara ya Watumishi wa Umma 65,394 yenye thamani ya shilingi bilioni
91,087,826,006.34 ambayo walikuwa wakidai kwa muda mrefu.
Sanjali na hilo, Mhe. Jenista amesema, Serikali imetumia
shilingi bilioni 1,330,306,572 kwa ajili ya kuwabadilisha kada na kuwalipa
mishahara Watumishi wa Umma 19,386.
Katika kuboresha huduma kwa wananchi, Mhe. Jenista amesema,
Serikali imeongeza rasilimaliwatu kwa kutoa vibali vya ajira mpya na mbadala12,336
vilivyogharimu jumla ya shilingi bilioni 7,761,869,809.
Aidha, Mhe. Jenista amesema, Serikali ya Awamu ya Sita
imewapunguzia Watumishi wa Umma asilimia moja (1%) ya makato ya PAYE kutoka
asilimia 9 hadi asilimia 8 lengo likiwa ni kuwapunguzia watumishi mzigo mkubwa
wa kodi hivyo kuwaongeza kiwango cha mshahara kinachobakia (Net salary)
kutokana na kupungua kwa kodi ya PAYE.
Hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita kuzingatia maslahi ya
Watumishi wa Umma kumewawezesha Watumishi wa Umma kuwa na morali ya utendaji
kazi yenye tija katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama akizungumza kwenye mkutano wake na Waandishi wa Habari uliolenga
kuuhabarisha umma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi
cha mwaka mmoja cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Sehemu
ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza kwenye mkutano wake na Waandishi wa Habari uliolenga kuuhabarisha
umma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha mwaka
mmoja cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment