Friday, March 25, 2022

MHE. JENISTA AWAASA MAAFISA WANAOSHUGHULIKIA MALALAMIKO YANAYOWASILISHWA KATIKA TAASISI ZA UMMA KUTOA MREJESHO KWA WAKATI

Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza

Tarehe 25 Machi, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka Maafisa wanaoshughulikia malalamiko yanayowasilishwa katika taasisi za umma kutoa mrejesho kwa wakati kwa wananchi na watumishi wa umma wanaowasilisha malalamiko katika taasisi hizo.

Akifunga mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) kwa Maafisa wanaoshughulikia malalamiko na Maafisa TEHAMA jijini Mwanza, Mhe. Jenista amesema katika eneo ambalo watumishi wa umma hawafanyi vizuri ni kutokutoa mrejesho wa malalamiko yanayowasilishwa katika taasisi za umma.

Mhe. Jenista amesema ni vizuri kutoa mrejesho hata kama lalamiko la mhusika liko kwenye hatua za kushughulikiwa ikiwa ni pamoja na kumueleza muda utakaotumika kulifanyia kazi lalamiko hilo na kuongeza kuwa, kwa malalamiko ambayo hayawezekani kutatuliwa kwa taratibu za kiutumishi, mlalamikaji ashauriwe kuliwasilisha kwenye vyombo vya kisheria ili aweze kupata haki yake.

“Eneo hili la ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi tukilisimamia vizuri, tutakuwa tumechangia kwa kiasi kikubwa kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista amesema mfumo wa eMrejesho ni mfumo pekee utakaochangia ushughulikiaji wa malalamiko kwa wakati na kuuboresha utumishi wa umma kuwa uliotukuka. 

Ameongeza kuwa, azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, ina matarajio kuwa watumishi wa umma wote wawe sehemu ya kutatua changamoto za Watanzania.

“Mfumo wa eMrejesho ukisimamiwa vizuri, utawapunguzia hata Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa kadhia ya kushughulikia malalamiko wanapokuwa katika ziara zao za kikazi kwani yatakuwa yameshughulikiwa na maafisa husika katika taasisi zetu.” Mhe. Jenista ameongeza.

Aidha, Mhe. Jenista ametoa maelekezo kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa mfumo wa eMrejesho kwa kuhakikisha watumishi wote wa taasisi wanatumia mfumo wa eMrejesho kikamilifu katika kushughulikia malalamiko na maoni ya wananchi na watumishi na kuzitaka taasisi zote za umma ziwe zimejiunga na mfumo huo ifikapo mwezi Septemba, 2022.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambaye ndiye mwenye jukumu la kusimamia utendaji kazi wa mfumo wa eMrejesho, Bi. Leila Mavika amesema mpaka sasa jumla ya watumishi 675 wameshapatiwa mafunzo ya kutumia mfumo huo na wako tayari kushughulikia malalamiko ya wananchi kama Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza mara kwa mara.

Watumishi hao waliopatiwa mafunzo wanatoka katika kanda zote nchini ambazo ni Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Maafisa wanaoshughulikia malalamiko na Maafisa TEHAMA kabla ya kufunga mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) kwa maafisa hao jijini Mwanza.


Maafisa wanaoshughulikia malalamiko na Maafisa TEHAMA wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kabla ya kufunga mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) kwa maafisa hao jijini Mwanza.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Ngusa Samike akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Maafisa wanaoshughulikia malalamiko na Maafisa TEHAMA alipokuwa akifunga mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) kwa maafisa hao jijini Mwanza.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika akielezea namna mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) yalivyofanyika kwa Maafisa wanaoshughulikia malalamiko na Maafisa TEHAMA jijini Mwanza kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufunga rasmi mafunzo hayo jijini Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitunuku cheti kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) kabla ya Mhe. Jenista kufunga rasmi mafunzo hayo yaliwashirikisha Maafisa wanaoshughulikia malalamiko na Maafisa TEHAMA jijini Mwanza.


Mwenyekiti wa mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho, Bw. Grant Patali akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya Waziri huyo kufunga rasmi mafunzo hayo jijini Mwanza.


 

No comments:

Post a Comment