Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 25 Machi, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, amezindua
Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Hali ya
Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma utakaoisaidia Serikali kupata
taarifa sahihi ya hali ya rasilimaliwatu kisayansi ili kuwapangia vituo vya
kazi watumishi kulingana na mahitaji ya huduma katika eneo husika.
Mhe. Jenista amesema
uzinduzi wa mfumo huo alioufanya jijini Dodoma ni sehemu ya utekelezaji wa azma
ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka Serikali yake kuwa na mifumo ya
kielektroniki itakayosimamia utendaji kazi wa watumishi na kuboresha utoaji wa
huduma kwa wananchi.
Mhe. Jenista
amethibitisha kuwa, mfumo huo umeshaanza kusaidia kukusanya, kuchakata na
kuchambua taarifa za watumishi kwa njia ya kisayansi zaidi ambao unaiwezesha
Serikali kutambua mahitaji halisi ya watumishi katika taasisi za umma.
“Mfumo huu utaisaidia
Serikali kuwa na tathmini ya kisayansi ya hali ya watumishi wa umma waliopo na
wanaohitajika kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali, hivyo Serikali
ikakuwa na takwimu sahihi zinazopatikana kupitia mfumo huu niliouzindua,” Mhe.
Jenista amefafanua.
Waziri Jenista amesema,
mfumo huo pia utasaidia Serikali kubaini taasisi ambazo zina watumishi wa ziada
ili kuwapeleka kwenye taasisi za umma ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi watakaowezesha
kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Mhe. Jenista
amewasisitiza na kuwaagiza waajiri wote katika taasisi za umma kuhakikisha
wanawasimamia wakurugenzi na wakuu wa idara zinazosimamia rasilimaliwatu,
kukamilisha wajibu wao wa kuingiza taarifa za watumishi katika mfumo huo.
Mhe. Jenista amezitaka
taasisi zote ambazo hazijakamilisha wajibu wa kuingiza taarifa za watumishi
kwenye mfumo huo kuhakikisha zinakamilisha zoezi hilo kabla ama ifikapo tarehe
31 Machi, 2022 na kuongeza kuwa, taasisi zitakazoshindwa kukamilisha zoezi hilo
zitakuwa zimekiuka maelekezo ya Serikali na zitachukuliwa hatua na mamlaka
husika.
Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kusanifu na kujenga
mifumo ya utendaji kazi ya TEHAMA itakayoongeza ufanisi wa taasisi za umma katika
kutoa huduma bora kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na viongozi wa Ofisi yake na Waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kieletroniki wa Tathmini ya Hali ya Watumishi wa Umma katika Taasisi za Umma uliofanyika jijini Dodoma.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama kuzungumza na waandishi wa habari wakati wa
uzinduzi wa Mfumo wa Kieletroniki wa Tathmini ya Hali ya Watumishi
wa Umma katika Taasisi za Umma uliofanyika jijini Dodoma. Wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara
ya TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango.
Baadhi ya Wakuu
wa Idara na Vitengo wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kieletroniki wa
Tathmini ya Hali ya Watumishi wa Umma katika Taasisi za Umma uliofanyika jijini
Dodoma.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akiwaonesha waandishi wa habari Taasisi zilizofanya vizuri
na ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye Mfumo wa Kieletroniki wa Tathmini ya Hali ya Watumishi wa Umma katika Taasisi za
Umma wakati akizindua mfumo huo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment