Thursday, April 29, 2021

MHE. MCHENGERWA AONGOZA MKUTANO WA PILI WA MAWAZIRI WA NCHI WANACHAMA WA UMOJA WA AFRIKA WALIORIDHIA MKATABA WA MAADILI NA MISINGI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA AFRIKA KWA NJIA YA MTANDAO

Na. Mary Mwakapenda-Dodoma

Tarehe 29 Aprili, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati Na.8 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati Na. 8 inayoshughulika na masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala leo ameongoza Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Maadili na Misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala Afrika kwa njia ya mtandao.

Mhe. Mchengerwa ameongoza Mkutano huo ili kupitia na kuidhinisha ajenda mbalimbali zilizowasilishwa na Mkutano wa Wataalamu uliofanyika tarehe 27 na 28 Aprili, 2021. 

Miongoni mwa ajenda zilizopitiwa na kuidhinishwa ni rasimu ya Nyenzo ya Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Miiko na Misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala Afrika; ambapo iliridhiwa kuwa Tanzania, Afrika ya Kusini, Namibia, Cameroon na Kenya zitahusika katika kufanya majaribio ya Utekelezaji wa Nyezo husika. 

Ajenda nyingine ni kuchagua Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba; ambapo walioidhinishwa ni Mwenyekiti kutoka Afrika Kusini, Makamu Mwenyekiti wa Kwanza kutoka Algeria, Makamu Mwenyekiti wa Pili kutoka Cameroon, Makamu Mwenyekiti wa Tatu kutoka Benin na Katibu kutoka Tanzania. 

Pia mkutano ulitathmini hali ya utiaji saini na uridhiwaji wa Mkataba wa Umoja wa Afrika na kupendekeza mbinu za kukuza uridhiaji wa pamoja wa Mkataba huo kwa nchi wanachama ambapo ilibainishwa kuwa, mpaka sasa mwenendo wa utiaji saini na uridhiwaji wa Mkataba miongoni mwa nchi wanachama, nchi 38 zimeshasaini, wakati nchi 19 tu zimeridhia na 19 zimewasilisha Nyaraka za kuidhinisha. 

Aidha, Mkutano uliridhia juu ya kuhimiza Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kusaini na kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika na Kuziomba AAPAM na AMDIN na Taasisi zingine kuutangaza Mkataba huu kupitia mijadala na tovuti mbalimbali. 

Sanjali na hilo, wajumbe walipitia na kuridhia Azimio la Mkutano wa Pili wa Nchi Wanachama kwa kuwasilisha taarifa ya kwanza ya utekelezaji wa Mkataba kwa Kamishna wa Umoja wa Afrika ifikapo mwezi Januari, 2022, na kuiomba Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuandaa taarifa ya jumla kuhusu Utendaji wa Utumishi wa Umma katika Afrika ikiwa ni pamoja na kudumisha ushirikiano na mshikamano baina ya Nchi Wanachama. 

Mkutano kazi huo, ulihudhuriwa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika walioridhia Mkataba huu ambao ni Algeria, Benin, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Mali, Namibia, Rwanda, Afrika ya Kusini, Mali, Ivory Coast, na Tanzania. Mkutano wa Tatu wa Nchi Wanachama utafanyika mwezi Aprili, 2022.

   


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati Na. 8 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati Na. 8 inayoshughulika na masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala akiongoza Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Maadili na Misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala Afrika kwa njia ya mtandao.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati Na. 8 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati Na. 8 inayoshughulika na masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa na Wajumbe wa Mkutano wa Wataalamu kutoka katika Ofisi yake, Bi Agnes kisaka Meena Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera (Wa kwanza kushoto kwake) na Bi Ellen Maduhu, Mkurugenzi Msaidizi wa Uchambuzi Sera wakati akiongoza Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Maadili na Misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala kwa njia ya mtandao.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati Na. 8 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati Na. 8 inayoshughulika na masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala akiwa na Wajumbe wa Mkutano wa Wataalamu kutoka katika Ofisi yake, Bi Agnes Kisaka Meena (Wa kwanza kushoto kwake) na Bi Ellen Maduhu, mara baada ya Mhe. Mchengerwa kuhitimisha Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Maadili na Misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala uliofanyika kwa njia ya mtandao.


 

TPSC NI TAASISI MUHIMU INAYOJENGA MAADILI NA UWEZO WA KIUTENDAJI KWA WATUMISHI WALIOPO NA WATAKAOAJIRIWA


Na. James K. Mwanamyoto-Mtwara

Tarehe 29 Aprili, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) ni taasisi muhimu ya kitaaluma yenye jukumu kubwa la kujenga maadili na uwezo wa kiutendaji kwa Watumishi wa Umma waliopo, wanaotarajiwa kuajiriwa na viongozi wateule wajao, hivyo watumishi wake wanapaswa kulinda hadhi ya chuo hicho kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kukiwezesha chuo hicho kufikia malengo yake.

Mhe. Ndejembi amesema hayo, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kampasi hiyo.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, TPSC ndio chuo pekee kinachojitofautisha na vyuo vingine kwa kutoa mafunzo yanayolenga kujenga maadili bora kwa Watumishi wa Umma waliopo, wanaotarajiwa kuajiriwa ili kuutumikia umma, ikiwa ni pamoja na viongozi wa umma wajao  watakaoteuliwa na mamlaka.

Ameongeza kuwa, Serikali ina dhamira ya kuhakikisha mhitimu kutoka chuo chochote cha ndani au nje ya nchi pindi anapotaka kuingia katika Utumishi wa Umma itamlazimu kupitia TPSC ili kufundishwa maadili na miiko ya Utumishi wa Umma kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amesema Kampasi ya Mtwara inatoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kutoa shauri za kitaalam na kufanya tafiti zenye tija ambazo zinatumiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, hivyo ametoa wito kwa taasisi za umma kuitumia kampasi hiyo kuwajengea uwezo kiutendaji watumishi wao.

Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara kilizinduliwa mwaka 2009 na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda, ambaye alielekeza TPSC iongeze kampasi mikoani ili kutoa huduma za mafunzo kwa Watumishi wa Umma waliopo na wanaotarajiwa kuajiriwa.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kampasi hiyo. 



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa hao. 

Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. 


Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa taarifa ya utekelezaji ya TPSC Kampasi ya Mtwara kwa Mhe. Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi ya Mtwara. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasili katika Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kampasi hiyo.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara mara baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kampasi hiyo.

 


 

UTUMISHI YAPATA MFANYAKAZI BORA WA MWAKA 2021

Na. Mary Mwakapenda-Dodoma

Tarehe 29 Aprili, 2021

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2021 kwa kuwashindanisha wafanyakazi bora watatu (3) kutoka Idara za Ofisi hiyo ambao wamepatikana kwa kigezo cha utendaji kazi mzuri kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio ya Utendaji Kazi (OPRAS).

Mfanyakazi bora aliyechaguliwa ni Bw. Steven Mgala kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.

Akizungumza na Watumishi wa Ofisi yake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amefafanua kuwa, wafanyakazi bora watatu (3) walioshindanishwa walipatikana baada ya mchujo wa Wafanyakazi bora 15 kutoka Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo utendaji kazi mzuri.

Mara baada ya wafanyakazi hao watatu kushindanishwa, Bw. Steven Mgala alipata ushindi akifuatiwa na Bw. Ally Ngowo kutoka Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ambapo hao wawili walishindanishwa tena, na Bw. Mgala kupata ushindi kwa mara nyingine.

Akimtangaza mshindi huyo, Dkt. Ndumbaro alimpongeza na kuwashukuru watumishi kwa kufanya uchaguzi uliozingatia vigezo.

Kabla ya kufanya uchaguzi, Dkt. Ndumbaro, aliwataka watumishi kumchagua mtumishi ambaye utendaji kazi wake unaonekana kuwa ni bora badala ya kuchagua kwasababu za kufahamiana.

“Tunapopiga kura, tusimchague mtumishi kwasababu unamfahamu au anatoka kwenye idara au kitengo kimoja, bali tumchague kwa utendaji kazi wake mzuri,” Dkt. Ndumbaro ameongeza.

Kwa upande wake, mfanyakazi bora aliyechaguliwa, Bw. Steven Mgala amewashukuru watumishi kwa kumuamini na kuona utendaji wake na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano kama kauli mbiu ya KAZI IENDELEE inavyohimizwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na Watumishi wa Ofisi yake na kutoa maelekezo ya namna ya kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2021 wa Ofisi yake. Kulia kwake ni Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Utumishi, Bi. Flora Nyela na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais UTUMISHI, Bw. Musa Joseph.



Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais UTUMISHI, Bw. Musa Joseph akimkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuzungumza na Watumishi wa Ofisi yake kabla ya kufanya uchaguzi wa mfanyakazi bora.

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akizungumza nao na kutoa maelekezo ya namna ya kumpata mfanyakazi bora wa ofisi wa mwaka 2021.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyekaa katikati) akishiriki zoezi la kuhesabu kura ili kumpata mfanyakazi bora wa Ofisi yake katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma. 



Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Utumishi, Bi. Flora Nyela, akitoa neno la shukrani na pongezi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alivyoendesha vizuri na kwa namna ya pekee zoezi la kumpata mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.


Mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Steven Mgala akitoa neno la shukrani kwa Watumishi baada ya kuchaguliwa kuwa Mfanyakazi bora wa Ofisi.



Mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Steven Mgala na Mfanyakazi bora aliyeshika nafasi ya pili, Bw, Ally Ngowo wakipongezana baada ya kushika nafasi hizo.

 

Wednesday, April 28, 2021

WANAOSIMAMIA ZOEZI LA UTAMBUZI NA UANDIKISHAJI KAYA MASKINI WATAKIWA KUTENDA HAKI


Na. James K. Mwanamyoto-Mtwara

Tarehe 28 Aprili, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini kutenda haki na kutokuwa na upendeleo wa aina yoyote wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo linaloendelea katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Mhe. Ndejembi amesema hayo kwa wawezeshaji wa zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuangalia namna zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini linavyoendeshwa katika manispaa hiyo.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa Mtaa, Mtendaji wa Mtaa na Mtendaji wa Kata ni viongozi muhimu wanaotegemewa na Serikali kusimamia kikamilifu zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini, ili kuondoa uwezekano wa kuwepo malalamiko ya upendeleo au kutotendewa haki kaya maskini ambazo ndio walengwa wakuu wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

 “Dirisha la utambuzi na uandikishaji likifungwa na zikaachwa kaya zinazostahili kupata ruzuku, kaya hizo zitaibua malalamiko na kuwasilisha malalamiko hayo Serikalini kupitia kwa Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi Watendaji jambo ambalo litatia doa azma ya Serikali ya kuziwezesha kaya maskini kuboresha maisha yao”, amehimiza Mhe. Ndejembi.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka waliopewa dhamana ya utambuzi na uandikishaji kaya maskini kuwa waadilifu kwa kuweka kando tofauti walizonazo na walengwa wa mpango wa TASAF ili kutenda haki, na kuongeza kuwa, hategemei kusikia kuna kaya yoyote maskini ambayo haijaandikishwa kutokana na sababu ya kutokuwa na uhusiano mzuri baina ya watendaji wa Serikali na walengwa.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Serikali kupitia Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 iliahidi kuboresha maisha ya kaya maskini nchini, hivyo kaya zote zenye sifa ya kupata ruzuku zitendewe haki kwa kuandikishwa, kinyume na hilo wasimamizi wa zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini watakuwa wanakwenda kinyume na azma ya Serikali.

Kwa upande wake, Meneja wa Uhawilishaji Fedha wa TASAF Bw. Selemani Masala amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na watendaji wanaosimamia zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Bw. Masala amesema, kitendo cha Mhe. Ndejembi kuwahimiza watendaji kutenda haki katika utambuzi na uandikishaji wa kaya kinawakumbusha watendaji hao kuwa waadilifu katika kutekeleza zoezi hilo.

Zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani linafanyika katika mitaa 75 ambayo haikuwepo kwenye Mapango wa Kunusuru Kaya Maskini kipindi cha kwanza. Ili kuhakikisha mitaa yote 75 inafikiwa, utambuzi umepangwa kufanyika kwa awamu nne kuanzia Aprili 25,  2021 na kukamilika Mei 6, 2021.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Bw. Hamisi Mkonga (wa kwanza kushoto) mkazi wa Mtaa wa Haikata, Manispaa ya Mtwara Mikindani aliyefanyiwa utambuzi ili kuandikishwa katika orodha ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wa pili kutoka kushoto) akielekea katika moja ya kaya maskini iliyopo Mtaa wa Haikata, Manispaa ya Mtwara Mikindani inayofanyiwa utambuzi ili kuandikishwa katika orodha ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisalimiana na baadhi ya Watendaji  wa Manispaa ya Mtwara Mikindani waliopewa jukumu la kufanya zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini zitakazonufaika na Mpango wa TASAF katika Manispaa hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa zoezi hilo.

 


Baadhi ya watendaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani waliopewa jukumu la kufanya zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini zitakazonufaika na Mpango wa TASAF katika Manispaa hiyo, wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa zoezi hilo.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani COL. Emmanuel Mwaigobeko akiwasilisha taarifa ya zoezi la utambuzi na uandikishaji wa Kaya Maskini kwa Mhe. Ndejembi, ambazo zitanufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa hiyo.


Meneja wa Uhawilishaji Fedha wa TASAF, Bw. Selemani Masala amemshukuru Mhe. Ndejembi (hayupo pichani) kwa kufanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na watendaji wanaosimamia zoezi la utambuzi na uandikishaji kaya maskini katika Manispaa ya Mtwara Mikindani. 


 

Tuesday, April 27, 2021

WAAJIRI ZINGATIENI MASILAHI YA WATUMISHI WA UMMA


Na. Veronica Mwafisi-Mtwara

Tarehe 28 Aprili, 2021


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kutoa kipaumbele kwenye masilahi ya watumishi, ikiwa ni pamoja kuwaasa Maafisa Utumishi kufanya ufuatiliaji ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata stahili zao kwa wakati.   

 Mheshimiwa Ndejembi ametoa wito huo kwa Waajiri na Maafisa Utumishi akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Manispaa hiyo.

 Akitoa mfano wa uzembe wa Afisa Utumishi mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mhe. Ndejembi amesema afisa huyo amesababisha watumishi wapatao 236 kutopata stahili ya kupandishwa madaraja kwa kisingizio cha kuchoka jambo ambalo halikubaliki katika Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, kitendo cha kutowapandisha madaraja watumishi hao kwa wakati kimewanyima haki yao ya msingi kwani katika Utumishi watalazimika kutengewa upya bajeti katika mwaka wa fedha mwingine ili waweze kupandishwa madaraja kwa mujibu wa sifa za miundo ya kada zao, ikiwa ni pamoja na kuzingatia uadilifu na utendaji kazi wao.

Sanjali na hilo, ameelezea kitendo cha waliokuwa Watumishi wa Umma katika Halimashuri ya Wilaya ya Kibaha ambao mpaka wanastaafu mwaka jana hawakupandishwa madaraja kwa wakati jambo ambalo limeathiri mafao yao.

Kutokana na changamoto ya watumishi hao kutopata stahili, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitomvumilia mwajiri au Afisa Utumishi yeyote atakayesababisha Watumishi wa Umma kutopata masilahi au stahili zao kwa wakati.

 “Tukibaini kuna Mwajiri au Afisa Utumishi yeyote anayezembea na kusababisha watumishi waliopo kwenye taasisi yake kukosa stahili zao kwa wakati, Serikali haitomvumilia kwani atakuwa anaharibu taswira nzuri ya ofisi yake ikiwa ni pamoja na taswira ya Mhe. Rais ambaye amehimiza Watumishi katika Taasisi zote za kupata stahili zao.

Kwa niaba ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Seleman Mzee amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwahimiza kutekeleza majukumu yao kikamilifu hususani suala la uzingatiaji wa masilahi ya Watumishi wa Umma mkoani Mtwara.

Mhe. Mzee ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliyowapewa na Mhe. Ndejembi mara watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi na kuongeza kuwa, watatoa kipaumbele kwenye suala la masilahi ya Watumishi wa Umma ili kuwajengea watumishi ari ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kutoa huduma bora kwa umma.

Mhe. Ndejembi, amefanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika Taasisi za Umma mkoani humo.

   


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi walio katika mkoa huo.

Baadhi ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi hao waliopo mkoani humo.


Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa ufafanuzi wa hoja za kiutumishi zilizowasiliswa na baadhi ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi na Viongozi walio katika mkoa huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bi. Changwa Mkwazu akiwasilisha hoja za kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi hao waliopo mkoani Mtwara.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akihimiza uadilifu kwa Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na Viongozi walio katika mkoa huo.

 


 

Sunday, April 25, 2021

Thursday, April 22, 2021

WABUNGE WAHIMIZWA KUWASILISHA KERO NA MALALAMIKO YANAYOHUSU UTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 22 Aprili, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewahimiza Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha kero na malalamiko ya kiutumishi yaliyo katika majimbo yao ili ofisi yake iweze kuyafanyia kazi.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/22 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili Bunge liweze kujadili na kuidhinisha.  

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, amedhamiria kuingoza ofisi yake kupunguza au kuyamaliza kabisa malalamiko ya Watumishi wa Umma na wananchi yanayohusu masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Akihimiza ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi, amewaelekeza Waajiri wote, hasa Maafisa Utumishi kuwasilisha madai ya watumishi kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa madeni ya watumishi yanayotokana stahili zao.

Ameongeza kuwa, Ofisi yake itaimarisha matumizi ya mfumo wa kushughulikia malalamiko katika Taasisi za Umma ili malalamiko ya watumishi na wananchi yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa Maafisa Utumishi kushughulikia changamoto za Watumishi wa Umma kwa wakati ili kujenga ari na morali ya watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa wananchi. 

“Mwajiri na Afisa Utumishi yeyote atakayeshindwa kutatua kero na malalamiko yaliyo ndani ya uwezo wake, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake”, amesisitiza Mhe. Mchengerwa.  

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma ili kuwajengea hali kiutendaji. 

Aidha, Mhe. Polepole ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya shilingi 727,932,861,000/= kwa ajili utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na taasisi zilizo chini yake.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litajadili ili kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/22 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yaliyowasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka 2021/22, Bungeni Jijini Dodoma leo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa, akizungumza na Naibu Waziri wa Ofisi yake, Mhe.Deogratius Ndejembi kabla ya kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka 2021/22, Bungeni Jijini Dodoma leo.



Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasilisha hoja Bungeni ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka 2021/22, Jijini Dodoma leo.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole akiwasilisha Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka 2021/22, Bungeni Jijini Dodoma leo.




 

Sunday, April 18, 2021

UTUMISHI KUSIMAMIA UTEKELEZAJI AHADI ZA MASUALA YA KIUTUMISHI KWENYE ILANI YA CCM YA MWAKA 2020


Na. James K. Mwanamyoto

Tarehe 18 Aprili, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Ofisi yake kusimamia utekelezaji wa ahadi za masuala ya kiutumishi na utawala bora zilizoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 ili kuhakikisha Sekta ya Umma inaimarika na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi yake uliofanyika jijini Dodoma.

Mhe. Ndejembi amelitaka baraza hilo kupitia na kuchambua Ilani kwa kina na kubaini ahadi zinazohusu Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Akihimiza utekelezaji wa Ilani katika Taasisi za Umma, amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza ahadi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi amesema, licha ya Watumishi wa Ofisi ya Rais-Utumishi kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza Ilani, lakini wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanabadili mtazamo hasi dhidi yao kwani malalamiko mengi yanayowasilishwa Utumishi yanatokana uzembe wa Watumishi wa Taasisi nyingine.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa baraza, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Bi. Agnes Meena amemuahidi Mhe. Ndejembi kuwa, Utumishi itahakikisha inaishauri vizuri Serikali kutekeleza Ilani na kuongeza kuwa, watumishi wataendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha ofisi kufikia malengo yake.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, ambapo Taasisi za Umma zinapaswa kukutana kupitia mpango na bajeti itakayowasilishwa Bungeni, kabla Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijapitisha bajeti husika kwa ajili ya utekelezaji.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa niaba ya Waziri mwenye Dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa.



Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati akifungua kikao cha Baraza hilo kwa niaba ya Waziri Mchengerwa.

Kaibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean akitoa neno la utngulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi yake. 


Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo. 



Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Bi. Agnes Meena akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI mara baada ya Naibu Waziri huyo kufungua kikao cha baraza hilo.

    

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI mara baada kufungua kikao cha baraza hilo kwa niaba ya Waziri Mchengerwa.



Saturday, April 17, 2021

WAZIRI MCHENGERWA AELEKEZA WATUMISHI NA VIONGOZI KUTAFUTIWA FURSA ZA MAFUNZO NDANI NA NJE YA NCHI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 17 Aprili, 2021 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameielekeza Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ya Ofisi yake kuhakikisha inawatafutia Watumishi wa Umma na Viongozi nafasi za mafunzo ya kuongeza maarifa na utaalamu ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo kiutendaji. 

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo, alipoitembelea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu yenye jukumu la kuandaa sera, miongozo na mifumo ya Usimamizi wa maendeleo ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwapatia mafunzo ya kutosha Watumishi wa Umma na Viongozi katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ili kuunga mkono azma hiyo ya Mhe. Rais, amesisitiza kuwa Ofisi yake kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu itahakikisha Watumishi wa Umma nchini wanapata mafunzo yatakayowajengea morali na hali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri Mchengerwa ameitaka Idara hiyo kuongeza jitihada za kutafuta Taasisi za Kitaifa na Kimataifa ambazo ziko tayari kutoa ufadhili wa mafunzo kwa Watumishi na Viongozi wa Taasisi za Umma na kuwasilisha fursa zilizopatikana kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI ili aone namna bora ya kuzitoa kwa walengwa kwa kuzingatia mahitaji ya Utumishi wa Umma na vipaumbele vya Serikali.

Aidha, amewataka Watumishi na Viongozi watakaopata fursa ya mafunzo kuwajengea uwezo Watumishi na Viongozi wengine ambao hawajabahatika kupata fursa ya mafunzo ili nao waweze kuboresha utendaji kazi wao.

Akipokea maelekezo ya Mhe. Mchengerwa, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bw. Elisante Mbwilo amesema Idara yake itaendelea kutafuta fursa za mafunzo kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili Watumishi na Viongozi wanufaike na fursa zitakazopatikana kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatekeleza jukumu la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 Kifungu G.1 (Kifungu kidogo cha 7, 9, 10 &11), Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 Kifungu cha 4.8 na Sera ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na watumishi wa ofisi yake waliopo UDOM mara baada ya kuwatembelea kwa lengo la kuhimiza Uwajibikaji. Kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Bw. Elisante Mbwilo (wa kwanza kushoto) mara baada ya kuwasili katika Ofisi yake iliyopo UDOM kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akielekea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ili kuona na kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo. Katikati ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitazama fomu za madai ya malimbikizo ya mishahara ya Watumishi wa Umma, mara baada ya kuitembelea Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini inayoshughulika na madai hayo. Kushoto ni Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro akishuhudia.


 

Friday, April 16, 2021

WATUMISHI WA UMMA TUMIENI JITIHADA BINAFSI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 16 Aprili, 2021 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma nchini kutumia jitihada binafsi katika kutekeleza majukumu yao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mhe. Ndejembi amesema ni vema Watumishi wa Umma wakatathmini mchango wao binafsi katika Utumishi wa Umma ili waweze kuwa na tija katika utoaji wa huduma kwa umma. 

“Ukiwa Mtumishi wa Umma uliyejitoa kuwahudumia Watanzania unapaswa kujiuliza unataka kufanya nini ili kutimiza malengo yako na ya Taasisi kwa ujumla,” Mhe. Ndejembi amesisitiza. 

Kuhusiana na madai mbalimbali ya kiutumishi, Mhe. Ndejembi amewaambia watumishi hao kuwa, wakati Serikali inayafanyia kazi madai yao ni vema wakatekeleza wajibu wao kikamilifu ili madai yao yawe na thamani inayolingana na huduma wanayoitoa. 

Aidha, amewasisitiza Wakuu wa Idara na Vitengo katika Taasisi za Umma kuwasilisha mpango kazi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi zao utakaoziwezesha Idara na Vitengo pamoja na Taasisi kutekeleza majukumu kikamilifu. 

Katika kuhimiza uwajibikaji unaozingatia maadili ya kiutumishi, Mhe. Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Chamwino Bw. Athman Masasi, kumpa barua ya onyo Mpima Ardhi wa Halmashauri hiyo, Bw. Charles Laseko kwa kosa la kushinikizwa na Afisa Usalama kuweka alama ya mpaka kwenye Kiwanja ambacho kimeuzwa na Jiji kwa mtu mwingine. 

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akisisitiza jambo kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 



Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akisikiliza hoja za Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.  


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akihoji utendaji kazi wa Mpima Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Bw. Charles Laseko (aliyesimama) anayetuhumiwa kumuwekea Afisa Usalama alama ya mpaka kwenye Kiwanja ambacho kimeuzwa na Jiji kwa mwananchi mwingine.