Tuesday, April 13, 2021

AFISA UTUMISHI ATAKAYESHINDWA KUTATUA KERO ZA WATUMISHI NA WANANCHI KUONDOLEWA KWENYE UTUMISHI WA UMMA

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 13 Aprili, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa amesema, iwapo Katibu Mkuu wa Ofisi yake na Naibu Waziri wake au yeye mwenyewe ataitembelea taasisi yoyote ya umma na kubaini Afisa Utumishi kashindwa kutatua kero za watumishi wa umma na wananchi wanaofuata huduma, atalazimika kumuondoa ili kumpa nafasi mtumishi mwingine mwenye uwezo wa kutoa huduma bora.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa ofisi yake kilichofanyika katika ofisi yake iliyopo Mtumba jijini Dodoma kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, ni dhamira ya Serikali kuwapa huduma stahiki watumishi wake pamoja na wananchi ambao ndio wameiamini na kuipa dhamana ya uongozi Serikali iliyopo madarakani ili ihakikishe wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

 

Kutokana na imani hiyo ya wananchi kwa Serikali, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa Maafisa Utumishi wote katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanasikiliza kero za watumishi na wananchi katika maeneo yao ya kazi, na kuongeza kuwa iwapo itabainika kuna Afisa Utumishi yeyote kashindwa kutatua kero zilizopo ndani ya uwezo wake ataielekeza mamlaka husika kusitisha ajira ya afisa huyo.

“Sitoweza kuvumilia kamwe uzembe wa aina yoyote unaomnyima haki mtumishi wa umma au mwananchi anayefuata huduma katika taasisi yoyote ya umma”, Mhe. Mchengerwa alisisitiza. 

Akizungumzia maelekezo ya Mhe. Waziri kuhusu utatuzi wa kero za Watumishi wa Umma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro ameilekeza Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma na Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kuainisha taasisi na halmashauri zenye malalamiko mengi ya watumishi ili aanze kufanyia kazi taasisi hizo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mchengerwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa, ofisi inaendelea na mchakato wa kuanzisha huduma ya CALL CENTRE itakayotoa fursa kwa watumishi na wananchi kupiga simu na kutuma ujumbe ili kutatuliwa kero na malalamiko yao ya kiutumishi.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi ameahidi kuwa, atashirikiana na Idara ya TEHAMA Serikalini kuandaa mfumo rafiki utakaowawezesha watumishi wa umma nchini kuwasilisha kero na malalamiko yao ili yafanyiwe kazi kwa wakati.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa amefanya kikao kazi chake cha kwanza na watumishi wa ofisi yake kwa lengo la kujitambulisha, kuhimiza uwajibikaji na kutoa maelekezo ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kuanisha azma yake ya kujenga Utumishi wa Umma wenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (Mb) akizungumza na watumishi wa ofisi yake iliyopo Mtumba jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (Mb) na watumishi wa ofisi yake chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (kushoto) akipokea Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake toka kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, mara baada ya waziri huyo kuzungumza na watumishi wa ofisi yake wakati wa kikao kazi cha kuhimiza uwajibikaji.


No comments:

Post a Comment