Thursday, April 29, 2021

UTUMISHI YAPATA MFANYAKAZI BORA WA MWAKA 2021

Na. Mary Mwakapenda-Dodoma

Tarehe 29 Aprili, 2021

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2021 kwa kuwashindanisha wafanyakazi bora watatu (3) kutoka Idara za Ofisi hiyo ambao wamepatikana kwa kigezo cha utendaji kazi mzuri kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio ya Utendaji Kazi (OPRAS).

Mfanyakazi bora aliyechaguliwa ni Bw. Steven Mgala kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.

Akizungumza na Watumishi wa Ofisi yake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amefafanua kuwa, wafanyakazi bora watatu (3) walioshindanishwa walipatikana baada ya mchujo wa Wafanyakazi bora 15 kutoka Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo utendaji kazi mzuri.

Mara baada ya wafanyakazi hao watatu kushindanishwa, Bw. Steven Mgala alipata ushindi akifuatiwa na Bw. Ally Ngowo kutoka Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ambapo hao wawili walishindanishwa tena, na Bw. Mgala kupata ushindi kwa mara nyingine.

Akimtangaza mshindi huyo, Dkt. Ndumbaro alimpongeza na kuwashukuru watumishi kwa kufanya uchaguzi uliozingatia vigezo.

Kabla ya kufanya uchaguzi, Dkt. Ndumbaro, aliwataka watumishi kumchagua mtumishi ambaye utendaji kazi wake unaonekana kuwa ni bora badala ya kuchagua kwasababu za kufahamiana.

“Tunapopiga kura, tusimchague mtumishi kwasababu unamfahamu au anatoka kwenye idara au kitengo kimoja, bali tumchague kwa utendaji kazi wake mzuri,” Dkt. Ndumbaro ameongeza.

Kwa upande wake, mfanyakazi bora aliyechaguliwa, Bw. Steven Mgala amewashukuru watumishi kwa kumuamini na kuona utendaji wake na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano kama kauli mbiu ya KAZI IENDELEE inavyohimizwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na Watumishi wa Ofisi yake na kutoa maelekezo ya namna ya kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2021 wa Ofisi yake. Kulia kwake ni Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Utumishi, Bi. Flora Nyela na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais UTUMISHI, Bw. Musa Joseph.



Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais UTUMISHI, Bw. Musa Joseph akimkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuzungumza na Watumishi wa Ofisi yake kabla ya kufanya uchaguzi wa mfanyakazi bora.

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akizungumza nao na kutoa maelekezo ya namna ya kumpata mfanyakazi bora wa ofisi wa mwaka 2021.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyekaa katikati) akishiriki zoezi la kuhesabu kura ili kumpata mfanyakazi bora wa Ofisi yake katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma. 



Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Utumishi, Bi. Flora Nyela, akitoa neno la shukrani na pongezi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alivyoendesha vizuri na kwa namna ya pekee zoezi la kumpata mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.


Mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Steven Mgala akitoa neno la shukrani kwa Watumishi baada ya kuchaguliwa kuwa Mfanyakazi bora wa Ofisi.



Mfanyakazi bora wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Steven Mgala na Mfanyakazi bora aliyeshika nafasi ya pili, Bw, Ally Ngowo wakipongezana baada ya kushika nafasi hizo.

 

No comments:

Post a Comment