Thursday, April 15, 2021

WAAJIRI SERIKALINI WATAKIWA KUWA NA MABARAZA YA WAFANYAKAZI YANAYOFANYA KAZI KIKAMILIFU

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 15 Aprili, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Waajiri katika Taasisi za Umma kuhahakisha wanakuwa na mabaraza hai ya wafanyakazi, yanayotekeleza wajibu wake kikamilifu ili kutoa haki ya ushirikishwaji kwa watumishi katika masuala muhimu yanayohusu ustawi wao. 

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa umma jijini Dodoma.

Mhe. Mchengerwa amesema, amelazimika kuwaelekeza waajiri kuwa na mabaraza hai ya wafanyakazi kwasababu amekuwa akipokea taarifa nyingi katika kipindi hiki kuwa yapo mabaraza yasiyofanya kazi wakati mabaraza yapo kwa mujibu wa sheria.

Ili kuhakikisha waajiri wanakuwa na mabaraza hai ya wafanyakazi, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuhakikisha katika mkutano wa baraza lijalo anampatia taarifa ya taasisi zote ambazo hazina mabaraza ya wafanyakazi kwani kutokuwa na mabaraza ni kuwanyima watumishi haki ya msingi ya kushirikishwa katika mambo muhimu yanayohusu mustakabali wa maendeleo yao ya kiutumishi. 

Sanjali na hilo, amemtaka Mwenyekiti wa Baraza kumpatia taarifa ya Mabaraza ya Wafanyakazi ambayo hayafanyi kazi na vikao kwa mujibu wa sheria kwani kuwa na mabaraza ni jambo moja na kufanya vikao ni jambo jingine, hivyo mabaraza lazima yafanyike ili kutekeleza wajibu wake.

Mhe. Mchengerwa amesititiza kuwa, ofisi yake itafuatilia kwa karibu na itachukua hatua stahiki iwapo itabaini kuna uzembe umefanywa na waajiri ili kukwamisha uwepo wa Mabaraza ya Wafanyakazi au utekelezaji wa majukumu ya Mabaraza hayo.

Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma limeundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 30 (1) (2) cha Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma SURA 105.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (katikati) akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dkt. Laurean Ndumbaro na kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza, Bi. Leah Ulaya.


Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano wa Baraza hilo jijini Dodoma.


Baadhi ya Wakurugenzi na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Mhe. Mchengerwa wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma.


Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma, Bi. Leah Ulaya akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Mchengerwa kwa niaba ya Wajumbe wa Baraza hilo mara baada ya Waziri huyo kufungua Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma. 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Ofisi yake, Dkt. Laurean Ndumbaro mara baada ya Waziri huyo kufungua Mkutano wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma.

 

No comments:

Post a Comment