Monday, January 30, 2023

WASHIRIKI WA KIKAO KAZI CHA KUTATHMINI MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA UZINGATIAJI WA MAADILI WATAKIWA KUTOA MAPENDEKEZO YATAKAYOIMARISHA UADILIFU KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 30 Januari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka washiriki wa kikao kazi cha kutathmini matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa umma kufanya uchambuzi yakinifu ili kutoa mapendekezo yatakayoiwezesha Serikali kuimarisha hali ya uzingatiaji wa maadili ya kiutendaji katika taasisi za umma.

Mhe. Jenista ametoa wito huo leo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa masuala ya maadili na utawala bora kilicholenga kufanya tathmini ya matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma kwa mwaka 2022. 

Mhe. Jenista amesema, lengo la Serikali kufanya tathmini ya matokeo ya hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma ni kupata mapendekezo thabiti yatakayosaidia kupunguza idadi ya taasisi ambazo zimebainika kuwa na changamoto ya watendaji wasiozingatia maadili.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mhe. Jenista amesema utafiti umeainisha kuwa Jeshi la Polisi, Mahakama na eneo la manunuzi, mikataba pamoja na huduma za ardhi ni maeneo yaliyokithiri vitendo ambavyo si vya kiadilifu.

“Nitoe wito kwenu washiriki wa kikao kazi hiki kuhakikisha mnafanya tathmini ya kina kuhusu matokeo hayo ya utafiti ili muainishe sababu za taasisi hizo kuendelea kuwa na viashiria vya ukiukaji wa maadili,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha tathmini ya matokeo ya hali ya uadilifu, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema, kikao kazi hicho kimeandaliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama ya kutaka kuandaliwa kwa kikao kazi cha wadau kitakachojadili taarifa ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022, maelekezo ambayo aliyatoa mnamo Disemba 09, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika amesema matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022 yataiwezesha Serikali kubaini maeneo ambayo taasisi za umma zimefanya vizuri na maeneo yenye mapungufu ili kuchukua hatua stahiki zitakazosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina ya matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa Umma ili kutoa mapendekezo yatakayokuwa na tija katika eneo la uzingatiaji wa maadili.

Wadau wanaoshiriki kikao kazi cha siku mbili cha kujadili matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022 ni Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa wizara, Wawakilishi wa Watendaji Wakuu wa Ofisi ya Bunge, Mahakama na Jeshi la Polisi, Wakurugenzi wa Taasisi Simamizi za Maadili, Wawakilishi wa Vyama vya Kitaaluma pamoja na Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.

Sehemu ya wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akifungua kikao kazi cha wadau hao kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Sehemu ya wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma wakiwa katika kikao kazi cha wadau hao kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022 kabla ya kufungua kikao kazi hicho jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika.


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika akielezea lengo la kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha wadau hao kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Mipango Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama baada ya Waziri huyo kufungua kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Sunday, January 29, 2023

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI KUPATIWA MAFUNZO YA AKILI YA KUHIMILI HISIA BINAFSI NA ZA WATEJA ILI WAWEZE KUTOA HUDUMA BORA

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 29 Januari, 2023

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema katika kuunga mkono kwa vitendo azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, ofisi yake inaandaa mafunzo ya akili ya kuhimili hisia binafsi na za wateja kwa watumishi wa ofisi yake ili kuwawezesha kutoa huduma bora.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa ofisi yake kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili wakati wa kutoa huduma kwa wadau na wananchi.

Dkt. Ndumbaro amewahimiza watumishi wa ofisi yake kuyatumia vizuri mafunzo ya kutoa huduma kwa kumjali mteja (customer care) waliyopatiwa ili kubadilika kiutendaji na kuwa na tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.                 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi ameungana na Dkt. Laurean Ndumbaro kwa kuwakumbusha watumishi wa ofisi yake kuwa, wanalo jukumu kubwa la kuwahudumia vizuri wananchi na wadau wa Utumishi wa Umma hivyo hawana budi kuitekeleza kwa vitendo dhana ya utoaji wa huduma kwa kumjali mteja.

Bw. Daudi amesisitiza kuwa, watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wanapaswa kuwa vinara wa kutoa huduma nzuri na bora kwa wateja, kwani ndiyo ofisi iliyokasimiwa jukumu la kusimamia utumishi wa umma nchini hivyo ndio kimbilio la utatuzi wa changamoto za watumishi wote wa umma pamoja na wananchi wanaofuata huduma katika taasisi za umma.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Musa Magufuli amesema, mafunzo ya huduma ya kumjali mteja waliyopatiwa wameyapokea vizuri na watayatumia kikamilifu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau na wananchi.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imepewa jukumu la usimamizi wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa mujibu wa Hati ya Mgawanyo wa madaraka iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tangazo la Serikali Na. 534 la tarehe 02 Julai, 2021. 

 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na watumishi wa ofisi yake jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau na wananchi. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu UTUMISHI Bw. Xavier Daudi (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Musa Magufuli (kulia).


 

Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa katika kikao kazi cha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi akizungumza na watumishi wa ofisi yake wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro na watumishi wa ofisi yake kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Katikati ni Katibu Mkuu UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Musa Magufuli (kulia).

 

 

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Musa Magufuli akieleza namna watumishi walivyoyapokea mafunzo ya customer care na kuahidi kuyatumia kikamilifu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau na wananchi.


 

Mmoja wa watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Mariam Salim akiwasilisha hoja kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu huyo na watumishi hao kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji.


 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akisikiliza hoja zinazowasilishwa na watumishi wa ofisi yake wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu UTUMISHI Bw. Xavier Daudi (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Musa Magufuli (kulia).


 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akitoa ufafanuzi wa hoja zilizowasilishwa na watumishi wa ofisi yake wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu UTUMISHI Bw. Xavier Daudi (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Musa Magufuli (kulia).