Wednesday, January 11, 2023

MWONGOZO WA KUDHIBITI VVU, UKIMWI NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA WAHUISHWA KULINDA AFYA ZA WATUMISHI ILI WAWE NA TIJA KATIKA TAIFA

 Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma

Tarehe 11 Januari, 2023

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agness Meena amesema Serikali imehuisha Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY) mahali pa kazi wa mwaka 2014 ili kulinda afya za watumishi wa umma, kuimarisha afya ya akili na kudhibiti msongo wa mawazo, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa watumishi katika kutoa huduma bora kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla. 

Bi. Meena amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu cha kupitia na kuthibitisha rasimu ya Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza (MYA) mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Bi. Meena amewaasa wakurugenzi hao, kutumia kikao kazi hicho kujadili na kutoa michango itakayoboresha rasimu ya mwongozo huo uliohuishwa, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwa na watumishi wenye afya nzuri ya akili na mwili itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Nawasihi mpitie kwa makini mwongozo huu ili mtoe maoni yatakayokidhi mahitaji ya sasa na baadae katika kukabiliana na changamoto za kiafya ambazo watumishi wa umma wamekuwa wakikabiliana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao, changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” Bi. Meena amesisitiza.

Bi. Meena ameongeza kuwa, mwongozo huo utasaidia Serikali kupunguza gharama za kuwahudumia watumishi wa umma wanaopata magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kupunguza vifo vya watumishi wa umma ili kulinda nguvukazi ya taifa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kinga na Mwitikio wa kitaifa dhidi ya VVU, Dkt. Hafidh Ameir amesema, endapo elimu itaendelea kutolewa kwa watumishi wa umma watapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI na watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujilinda dhidi ya maambuzi ya VVU ikiwa ni pamoja na kwa hiari yao kumueleza mwajiri kuwa wanaishi na virusi vya UKIMWI na hatimaye kupatiwa huduma stahiki. 

Dkt. Ameir amesema, bado kuna baadhi ya watu wanadhani mtu mwenye virusi vya UKIMWI anaweza kumuambukiza mtu mwingine kwa kupiga chafya, kuchangia vyombo na vifaa vya kazi hivyo kuna kazi ya ziada kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya kazi. 

Naye, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uchambuzi Sera, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Charles Kato amesema, Mwaka 2014 ilionekana kuna umuhimu wa kujumuisha magonjwa sugu yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiendelea kuisumbua jamii wakiwemo watumishi wa umma ambayo ndio sababu pia iliyofanya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kupitia Idara ya Uendelezaji Sera kukutana na Wakurugenzi wa Utumishi na Utawala ili kupitia na kuthibitisha rasimu hiyo ya Mwongozo wa VVU na Ukimwi.  

Dkt. Kato amesema, utumishi wa umma unakabiliwa na changamoto ya uwepo wa magonjwa yasiombakuza ambayo yanaathiri utendaji kazi, hivyo Ofisi ya Rais-UTUMISHI kupitia Idara ya Uendelezaji Sera iliona kuna umuhimu wa kukutana na Wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu ili kupitia na kuthibitisha rasimu ya Mwongozo wa VVU na UKIMWI uliohuishwa ili uweze kuwa na tija na manufaa katika kulinda rasilimaliwatu Serikalini.  

Kikao kazi hicho cha siku moja kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Idara ya Uendelezaji Sera kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara mbalimbali.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agness Meena akizungumza na Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu walioshiriki kikao kazi cha kujadili Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza mahali pa kazi kilichofanyika jijini Dodoma. 


Sehemu ya wadau kutoka katika Wizara mbalimbali wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agness Meena (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi cha kujadili Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza mahali pa kazi kilichofanyika jijini Dodoma. 


Mratibu wa Kinga na Mwitikio wa kitaifa dhidi ya VVU, Dkt. Hafidh Ameir akitoa taarifa ya hali ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agness Meena (hayupo pichani) kufungua kikao kazi cha kujadili Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza mahali pa kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uchambuzi Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Charles Kato   akitoa neno la utangulizi kabla ya Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agness Meena kufungua kikao kazi cha kujadili Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza mahali pa kazi kilichofanyika jijini Dodoma. 


Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Mwanaamani Mtoo akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Ujumuishwaji wa Anuai za Jamii mahali pa kazi wakati wa kikao kazi cha kujadili Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza kilichofanyika jijini Dodoma. 



No comments:

Post a Comment