Sunday, January 15, 2023

MFUKO WA UWEKEZAJI WA PAMOJA WA ‘FAIDA FUND’ UMELENGA KUWANUFAISHA WATANZANIA WA KIPATO CHA CHINI, KATI NA CHA JUU

 Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 15 Januari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND umeanzishwa kwa lengo la kuwanufaisha watanzania wote wa kipato cha chini, kati na cha juu ambao wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya kupata mtaji wa kuwekeza kwenye masoko ya fedha na mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kuzindua Mfuko wa Faida (FAIDA FUND) unaoratibiwa na Watumishi Housing Investments (WHI).

Mhe. Jenista amesema kuwa, Mfuko wa Faida unatarajia kutoa gawio kubwa litakalokuwa na tija kwa wote ambao watawekeza kwenye Mfuko wa Faida kwa lengo la kujikwamua kiuchumi, hivyo elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kununua vipande katika mfuko huo.

“Mfuko wa Faida ni salama  kwa wawekezaji ambao wanataka kuepuka upotevu wa fedha, hivyo natoa wito kwa wanawake, vijana, wazee  na makundi mengine maalum kujitokeza  kununua vipande ili wanufaike na uwekezaji katika mfuko huu,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Sanjari na hilo, Mhe. Jenista ametoa wito kwa watumishi wa umma, wanachama wa mifuko ya hifadhi za jamii na watanzania wote kujitokeza na kuwekeza katika Mfuko wa Faida ili wapate kipato kitakachoboresha shughuli zao za kiuchumi na maisha yao kwa ujumla.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista kuzindua Mfuko wa Faida kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amempongeza Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro kwa kuisimamia vema WHI kujenga mfumo rafiki uliowawezesha wananchi kuwekeza kwenye mfuko huo ambao hivi sasa kiasi cha shilingi bilioni 13.5 kimewekezwa. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ametoa wito kwa watumishi wa umma nchini kuwekeza katika Mfuko wa Faida kwani unatoa fursa ya kuwekeza kidogo kidogo kuanzia shilingi 10,000/= na kuongeza kuwa, watumishi wakinunua vipande vitawawezesha kupata gawio na ikifika wakati wa kustaafu watakuwa na akiba ya kutosha itakayowasaidia kuendesha maisha yao. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba amesema katika kutekeleza maelelezo ya Mhe. Rais ya kujenga mifumo rafiki ya TEHAMA ya utoaji huduma kwa wananchi, eGA kwa kushirikiana na WHI imejenga mfumo unatoa fursa kwa wananchi walio pembezoni kujisajili na kuwekeza kwenye Mfuko wa Faida kupitia simu za kiganjani ili wapate fursa ya kuwekeza kama wanayoipata wananchi wanaoishi mjini.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI) Dkt. Fred Msemwa ameishukuru Benki ya CRDB ambayo ndio msimamizi wa dhamana ya Mfuko wa Faida, kwa weledi wake kiutendaji katika kusimamia  jukumu hilo na hatimaye wananchi waliowekeza kunufaika na FAIDA FUND.

Aidha, Dkt. Msemwa ameishukuru Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kushirikiana na taasisi yake kuujenga Mfuko wa Faida, na kuongeza kuwa ushirikiano walioutoa, ubunifu na weledi wa mamlaka hiyo umeiwezesha WHI kujenga Mfuko wa Faida wenye tija kwa watanzania.

FAIDA FUND ni mpango ulio wazi unaotoa fursa ya uwekezaji kwa watanzania hasa wa kipato cha kati na cha chini kupitia uwekezaji katika vipande ili kupata mapato shindani kupitia ukuaji wa mitaji, mapato yaliyotokana na  utamaduni wa kuwekeza katika masoko ya fedha na mitaji.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wadau wa Watumishi Housing Investments (WHI) jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na WHI kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwenye mfuko huo ili kupata mtaji utakaoboresha maisha yao.


Baadhi ya wadau wa Watumishi Housing Investments (WHI) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND uliofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa J.K Nyerere. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wadau wa Watumishi Housing Investments (WHI) wakati wa hafla ya uzinduzi wa  mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na WHI. 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa utambulisho wa Viongozi wa Serikali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuuzindua mfuko huo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifuatilia Makala fupi inayoelezea   namna mfumo wa FAIDA FUND unavyofanya kazi. Wengine ni Viongozi mbalimbali na wadau wa Watumishi Housing Investiments (WHI).


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizindua mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwenye mfuko huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizindua mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwenye mfuko huo. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi cheti kwa mmoja wa wawekezaji wa mfuko wa FAIDA FUND ulioanzishwa na Watumishi Housing Investments (WHI) ili kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwenye mfuko huo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa Watumishi Housing Investments (WHI) mara baada ya waziri huyo kuzindua mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na WHI.

 



No comments:

Post a Comment