Na. Veronica Mwafisi – Geita
Tarehe 27 Januari, 2023
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi amewaasa watumishi wa umma nchini katika maeneo yao ya kazi
kuhakikisha wanalinda na kusimamia fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza miradi mbalimbali
ya maendeleo ili iwanufaishe Watanzania na taifa kwa ujumla.
Mhe.
Ndejembi ametoa wito huo, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Geita akiwa kwenye
ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa umma walio katika halmashauri hiyo.
Mhe. Ndejembi amewataka watumishi
kutokuwa na tamaa ya kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa manufaa yao
binafsi kwani kitendo hicho kinakwamisha jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan za kuliletea taifa maendeleo.
“Tuache tabia ya kudokoa fedha za
miradi ya maendeleo kwani jukumu la kulinda fedha hizo ni la watumishi wa umma
wote si la viongozi pekee,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Akizungumzia
kuhusu watumishi wa umma kutoa elimu juu ya jitihada za kuleta maendeleo
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, Mhe. Ndejembi amewataka watumishi wa
umma kutoa elimu kwa wananchi wanaowahudumia ili waelewe azma ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutafuta fedha
za kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
“Ni wajibu wetu kumsemea Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa yale mema ambayo analifanyia taifa kupitia utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo,”Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Halmashauri wa Wilaya ya Geita Bw. Charles Kazungu ameishukuru Serikali kwa
namna inavyowajali wananchi wa Geita kwa kuwapelekea fedha nyingi kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameendelea
na ziara yake ya kikazi Mkoani Geita kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika
halmashauri hiyo.
Watumishi wa Umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Geita
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji
na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.
Katibu
Tawala wa Wilaya ya Geita, Bw. Thomas
Dimme akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Geita (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri
huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi wa umma katika halmashauri hiyo.
Mtumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Geita, Bw. Evarist Kimori akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi
wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment