Monday, January 30, 2023

WASHIRIKI WA KIKAO KAZI CHA KUTATHMINI MATOKEO YA UTAFITI WA HALI YA UZINGATIAJI WA MAADILI WATAKIWA KUTOA MAPENDEKEZO YATAKAYOIMARISHA UADILIFU KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 30 Januari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka washiriki wa kikao kazi cha kutathmini matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa umma kufanya uchambuzi yakinifu ili kutoa mapendekezo yatakayoiwezesha Serikali kuimarisha hali ya uzingatiaji wa maadili ya kiutendaji katika taasisi za umma.

Mhe. Jenista ametoa wito huo leo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa masuala ya maadili na utawala bora kilicholenga kufanya tathmini ya matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma kwa mwaka 2022. 

Mhe. Jenista amesema, lengo la Serikali kufanya tathmini ya matokeo ya hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma ni kupata mapendekezo thabiti yatakayosaidia kupunguza idadi ya taasisi ambazo zimebainika kuwa na changamoto ya watendaji wasiozingatia maadili.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mhe. Jenista amesema utafiti umeainisha kuwa Jeshi la Polisi, Mahakama na eneo la manunuzi, mikataba pamoja na huduma za ardhi ni maeneo yaliyokithiri vitendo ambavyo si vya kiadilifu.

“Nitoe wito kwenu washiriki wa kikao kazi hiki kuhakikisha mnafanya tathmini ya kina kuhusu matokeo hayo ya utafiti ili muainishe sababu za taasisi hizo kuendelea kuwa na viashiria vya ukiukaji wa maadili,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha tathmini ya matokeo ya hali ya uadilifu, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema, kikao kazi hicho kimeandaliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama ya kutaka kuandaliwa kwa kikao kazi cha wadau kitakachojadili taarifa ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022, maelekezo ambayo aliyatoa mnamo Disemba 09, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika amesema matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022 yataiwezesha Serikali kubaini maeneo ambayo taasisi za umma zimefanya vizuri na maeneo yenye mapungufu ili kuchukua hatua stahiki zitakazosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina ya matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa Umma ili kutoa mapendekezo yatakayokuwa na tija katika eneo la uzingatiaji wa maadili.

Wadau wanaoshiriki kikao kazi cha siku mbili cha kujadili matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022 ni Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa wizara, Wawakilishi wa Watendaji Wakuu wa Ofisi ya Bunge, Mahakama na Jeshi la Polisi, Wakurugenzi wa Taasisi Simamizi za Maadili, Wawakilishi wa Vyama vya Kitaaluma pamoja na Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.

Sehemu ya wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akifungua kikao kazi cha wadau hao kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Sehemu ya wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma wakiwa katika kikao kazi cha wadau hao kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022 kabla ya kufungua kikao kazi hicho jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika.


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika akielezea lengo la kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha wadau hao kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Mipango Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama baada ya Waziri huyo kufungua kikao kazi cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.


No comments:

Post a Comment