Wednesday, February 1, 2023

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUANDAA NA KUHUISHA MIKATABA YA HUDUMA KWA MTEJA NA KUIWASILISHA UTUMISHI ILI KUPATA IDHINI YA KUITUMIA

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 01 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezitaka Taasisi za Umma kote nchini kuwa na Mitakaba ya Huduma kwa Mteja iliyohuishwa na kuiwasilisha katika ofisi yake kwa ajili ya ukaguzi na idhini ya kuitumia, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi, wadau na wawekezaji.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na Vyombo vya Habari kulezea lengo la Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Taasisi za Umma zinazotoa huduma bora kwa wananchi, wadau na wageni wanaokuja nchini kuwekeza.

Mhe. Jenista amesema kuwa, mara baada ya ofisi yake kuidhinisha mikataba hiyo kwa ajili ya kuanza kutumika, taasisi zinapaswa kuitangaza ili kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu huduma, viwango vya huduma, na muda wa kutoa huduma hizo katika taasisi husika.

Aidha, Mhe. Jenista amezielekeza taasisi za umma ambazo mikataba yake ya Huduma kwa Mteja itaidhinishwa na ofisi yake, kuendelea  kufanya ufuatiliaji na  tathmini ya viwango vya utoaji wa huduma vilivyoainishwa katika mikataba yao ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya maboresho stahiki katika michakato ya utoaji wa huduma.

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, mikataba itakayoidhishwa na ofisi yake baada ya kukidhi vigezo itazinduliwa kwa pamoja kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itakuwa ni tarehe 28 Februari, 2023   ikihusisha mikataba ya Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na uzinduzi wa awamu ya pili utafanyika tarehe 28, Aprili, 2023 ukihusisha mikataba ya Wakala za Serikali, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma pamoja na taasisi nyingine za Serikali.

“Taasisi zote zilizo katika makundi hayo niliyoyataja zinatakiwa kuwasilisha nakala za Mikataba ya Huduma kwa Mteja, Ofisi ya Rais-UTUMISHI wiki mbili kabla ya tarehe ya uzinduzi ili ofisi yangu ipate muda wa kuikagua na kujiridhisha kama ina viwango vinavyotarajiwa, hivyo nawasisitiza waajiri kuzingatia agizo hili,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni ahadi ya kimaandishi kati ya taasisi ya umma na mteja wake, ambao unamuwezesha mteja huyo kufahamu huduma zinazotolewa na taasisi husika, viwango vya utoaji wa huduma, wajibu wa taasisi husika, wajibu na haki ya mteja anayepokea huduma, ikiwa ni pamoja na kufahamu njia zitakazomuwezesha mteja kupokea huduma na kutoa mrejesho wa huduma aliyopatiwa na taasisi husika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) jijini Dodoma kuelezea utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika Taasisi za Umma nchini.

 

Sehemu ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao jijini Dodoma kuelezea utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika Taasisi za Umma nchini.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika Taasisi za Umma nchini. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi na Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda.

 

 

Waandishi wa Habari na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakiwa katika kwenye mkutano na wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Vyombo vya Habari jijini Dodoma alipokuwa akielezea utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika Taasisi za Umma nchini.


 

 

No comments:

Post a Comment