Na. Veronica E. Mwafisi-Iringa
Tarehe 18 Februari, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amezitaka
Taasisi za umma nchini kuishirikisha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
kutengeneza mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma kwa umma ili iweze kukidhi
mahitaji na viwango katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo
hayo alipotembelea ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa lengo la kukagua utendaji
kazi wake na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo.
Mhe. Ndejembi amesema, Mamlaka
ya Serikali Mtandao ipo tayari kushirikiana na taasisi za umma kusanifu mifumo,
hivyo amezihimiza taasisi zote zenye nia ya kutengeneza mifumo, kuhakikisha
zinaishirikisha eGA ili kutimiza
malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya kuwa na serikali ya kidijitali.
“Taasisi za umma itumieni Mamlakaka ya
Serikali Mtandao (eGA) ipasavyo kutengeneza
mifumo itakayokidhi viwango vya kutoa huduma bora kwa wananchi kwa lengo la kutimiza
azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwa na serikali mtandao,” Mhe. Ndejembi
amesisitiza.
Akizungumzia maeneo ambayo
jiografia yake haipo vizuri, Mhe. Ndejembi amesema maeneo hayo yanapaswa kuwa
na miundombinu ya TEHAMA itakayowezesha upatikanaji wa huduma za kimtandao zilizosanifiwa
na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Katika kukabiliana na
changamoto za kijiografia zinazokwamisha utoaji huduma kwa umma, Mhe. Ndejembi ametoa
wito kwa eGA kutumia ubunifu na
weledi wake kusanifu mifumo itakayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa, taasisi za serikali 14 zimehifadhi
mifumo yake katika kituo kilichopo Mamlaka ya
Serikali Mtandao (e-GA) Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini ambapo jumla ya mifumo 189 imehifadhiwa ikiwemo GePG, GMS,
e-office, e-vibali, m-government na mingineyo.
Mhandisi Ndomba amesema,
Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
kupitia mpango mkakati wa 2021/2022 hadi 2025/2026 imejipanga kuongeza vituo
vya ubunifu vingine zaidi ili kuboresha utoaji huduma kwa taasisi za umma zinazotaka
kutengeneza mifumo ya TEHAMA.
Aidha, Mhandisi Ndomba,
amemshukuru Naibu Waziri Ndejembi kwa kutembelea Ofisi ya Mamlaka ya Serikali
Mtandao Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani
Iringa kwa lengo la kukagua utendaji kazi wake na kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa ofisi hiyo.
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, kwa lengo la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza na
watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Iringa alipotembelea
ofisi hiyo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu na kuhimiza uwajibikaji
kwa watumishi hao.
Sehemu ya watumishi wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (meza kuu
katikati) wakati akizungumza nao kwenye ofisi hiyo mkoani Iringa kwa lengo la
kukagua utekelezaji wa majukumu na kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba (aliyesimama)
akielezea majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) kabla
ya Naibu Waziri huyo kuzungumza na watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
mkoani Iringa alipotembelea ofisi hiyo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa
majukumu na kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(katikati) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
Mhandisi Benedict Ndomba (wa kwanza kulia) wakati akifafanua jambo kwa Naibu
Waziri huyo alipotembelea ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani
Iringa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu na kuhimiza uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment