Thursday, February 9, 2023

eGA YATAKIWA KUENDELEA KUFANYA TAFITI NA KUBUNI MIFUMO ITAKAYOIMARISHA MATUMIZI YA TEHAMA KAMA ILIVYOELEKEZWA NA RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

 

Na. James K. Mwanamyoto-Arusha

Tarehe 09 Februari, 2023           

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameielekeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuendelea kufanya tafiti na kubuni mifumo ya TEHAMA itakayoimarisha utendaji kazi Serikalini ili kuendana na kasi ya dunia katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Tatu cha Serikali Mtandao jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kinachoratibiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mhe. Ndejembi amesema, maelekezo ya kuitaka eGA kubuni mifumo ya TEHAMA, yamelenga kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka Taasisi za Umma nchini kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili taifa liendane na kasi ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambayo yanachagizwa na TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

 “eGA endeleeni kufanya tafiti na kubuni mifumo ya TEHAMA itakayoliwezesha taifa kuwa na utumishi wa umma imara pamoja na kuimarisha sekta za viwanda, biashara na uwekezaji,” Mhe. Ndejembi amehimiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amezipongeza taasisi za umma ambazo tayari zimeanza kutumia mifumo ya TEHAMA kutoa huduma kwa wananchi na kuzitaja taasisi hizo kuwa ni PSSSF, TANESCO, BRELLA na HESLB na kutoa wito kwa taasisi nyingine za umma kuiga mfano huo ili kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha matumizi ya serikali mtandao.

Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo ambayo yataiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita kutimiza lengo la kuimarisha matumizi ya serikali mtandao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi jambo ambalo ndio kipaumbele cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kuwa, washiriki wa kikao kazi hicho ndio wenye jukumu na dhamana kubwa ya kutimiza lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuijenga serikali mtandao itakayotoa huduma bora kwa wananchi.

“Nitoe wito kwenu wakuu wa taasisi, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri na watendaji wa Serikali mnaoshiriki kikao kazi hiki, kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anajipanga kuiwezesha taasisi yake kuwa ya kidijitali,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Dkt. Ndumbaro amesema, Ofisi yake imedhamiria kuwa, alama mojawapo atakayoiacha Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iwe ni kuibadili serikali kuwa ya kidijitali na kuongeza kuwa, ili kufikia azma hiyo inampasa kila mshiriki kuunga mkono kwa vitendo lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwa na serikali mtandao yenye tija katika utoaji huduma kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Mhandisi Benedict Ndomba amesema eGA imeendelea kusimamia na kuhimiza uzingatiaji wa sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na kutoa kutoa viwango na miongozo ya kiufundi kuhusu utekelezaji wa serikali mtandao ili kuhakikisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma yanakuwa na tija katika kuboresha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kikao kazi hicho cha tatu cha Serikali Mtandao kinachofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 08 hadi 10 Februari, 2023 kinaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 10 ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) toka kuanzishwa kwake.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na washiriki wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao wakati akifungua kikao kazi hicho jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

 

Washiriki wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao wakisikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati akifungua kikao kazi hicho jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufungua kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao jijini Arusha.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba akieleza majukumu yaliyotekelezwa na mamlaka yake wakati wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao kilichofunguliwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi jijini Arusha.

 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa taasisi za umma (waliosimama) na viongozi (waliokaa) mara baada ya kufungua kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

 


No comments:

Post a Comment