Thursday, February 16, 2023

MHE.JENISTA ASISITIZA UTEKELEZAJI MKAKATI WA KUSHUGHULIKIA RUFAA ZA WATUMISHI NA WA KUZUIA ONGEZEKO LA MASHAURI YA KINIDHAMU

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 16 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza mpango mkakati wa kushughulikia rufaa za watumishi wa umma kwa wakati pamoja na kuandaa na kutekeleza mpango mkakati utakaowawezesha waajiri kupunguza ongezeko la mashauri ya kinidhamu yanayowasilishwa Tume ya Utumishi wa Umma kufanyiwa maamuzi.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma kilicholenga kuhimiza ufanisi wa utendaji kazi wa Tume hiyo.

Mhe. Jenista amesema, rufaa zikifanyiwa kazi kwa wakati, Tume itakuwa imetenda haki kwa watumishi wenye mashauri ya kinidhamu, na kuongeza kuwa mashauri ya kinidhamu yasiposhughulikiwa kwa wakati watumishi wanapoteza haki zao na waajiri wanapoteza haki ya kumuadhibu mtumishi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za kiutumishi zilizopo.

“Ushughulikiaji wa rufaa ukifanyika kwa wakati, mtumishi atakuwa ametendewa haki ya kutoadhibiwa anapobainika kutotenda kosa na haki ya kuadhibiwa baada ya kuthibitika kutenda kosa,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, mashauri ya kinidhamu yakichukua muda mrefu, Serikali inaingia gharama kuyaendesha na watumishi wanaokabiliwa na mashauri ya kinidhamu wanakosa tija kiutendaji kwasababu muda mwingi wanautumia kufuatilia mashauri yao badala ya kufanya kazi.

Mhe. Jenista amesema, Tume ya Utumishi wa Umma ikitekeleza majukumu yake ipasavyo italisaidia taifa kutenda haki kwa mtumishi wa umma na kuepuka kuingia gharama kubwa ya uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu ili kuokoa fedha za umma.

Aidha, Mhe. Jenista ameipongeza Tume ya Utumishi wa Umma kwa uamuzi wa kutengeneza mfumo wa ushughulikiaji wa rufaa na malalamiko ambao utakuwa na uwezo wa kuzifikia kwa wakati mamlaka zote za ajira katika utumishi wa umma na kuongeza kuwa, kuwepo kwa mfumo huo ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu na ndio maana amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Tume hiyo kuwezesha mfumo ukamilike kwa wakati na uanze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma, Naibu Katibu, Idara ya Rufaa na Malalamiko ya Tume hiyo, Bw. John Mbisso amemhakikishia Mhe. Jenista kuwa watatekeleza ipasavyo mkakati wa kushughulikia malalamiko na rufaa ikiwa ni pamoja na kuandaa mkakati wa kuzuia ongezeko la mashauri ya kinidhamu kama alivyowaelekeza.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo la kuandaa mfumo wa ushughulikiaji wa rufaa na malalamiko, Bw. Mbisso amesema agizo litatekelezwa kikamilifu kwani mfumo ukikamilika utasaidia kupunguza malalamiko yanayotokana na mchakato wa ushughulikiaji  wa malalamiko na mashauri ya kinidhamu yaliyowasilishwa Tume ya Utumishi wa Umma.

Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu kubwa la kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za rasilimaliwatu katika taasisi za umma na kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unaendeshwa  kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti hiyo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji.

                                     


 

Sehemu ya watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na watendaji hao kilicholenga kuhimiza uwajibikaji.

                                 

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama (Aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (katikati) wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Menejimenti ya tume hiyo kilichofanyika jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu, Idara ya Rufaa na Malalamiko, Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso.

 

 

Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Sylvester Koko (Katikati) akimuonesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Wa kwanza kulia) mpango kazi wa kutekeleza mradi wa ujenzi wa mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa rufaa na malalamiko wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na menejimenti ya tume hiyo kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama.

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Meza kuu katikati) akisisitiza jambo kwa Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa kikao kazi chake na menejimenti hiyo kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

 


 

Naibu Katibu, Idara ya Rufaa na Malalamiko, Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso (aliyesimama) akitoa neno la shukrani mara baada ya   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuhitimisha kikao kazi chake na menejimenti ya tume hiyo kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.


 

 

No comments:

Post a Comment