Saturday, February 4, 2023

OFISI YA RAIS-UTUMISHI KUSHIRIKIANA NA TUME YA HAKI ZA BINADAMU KUJENGA UTAMADUNI WA KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU, MISINGI YA UTAWALA BORA NA UTU WA MTU


Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 04 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ili kuiwezesha Tume hiyo kutekeleza dira ya kujenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu, kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kusimamia haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu. 

Mhe. Jenista ametoa ahadi hiyo jijini Dodoma, wakati akizungumza na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora waliomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kubadilisha uzoefu wa utendaji kazi katika kusimamia eneo la utawala bora nchini. 

Mhe. Jenista amesema, ni muhimu kwa ofisi yake kushirikiana kikamilfu na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili iwe sehemu ya kuiwezesha Tume hiyo kuwa taasisi ya kitaifa ambayo ni kitivo cha kukuza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini. 

“Niwahakikishie kwamba, ofisi yangu ipo tayari kushirikiana nanyi katika utekelezaji wa majukumu ya Tume, kwani ushirikiano katika kuimarisha misingi ya utawala bora kwenye utumishi wa umma ni eneo mojawapo tunalotoa kipaumbele,” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Akitambua mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha utawala bora nchini, Mhe. Jenista amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusimamia kikamilifu maslahi na stahiki za watumishi wa umma kitendo ambacho kimewawezesha watumishi wa umma nchini kutambua wajibu wao katika kutoa haki na kusimamia misingi ya utawala bora pindi wanapotekeleza jukumu la kuwahudumia wananchi. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu, amesema ofisi yake imedhamiria kuendelea kujenga mahusiano kiutendaji na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kutoa mchango katika kuimarisha utawala bora nchini. 

Mhe. Mwaimu amesema, ushirikiano wa Tume yake na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora utasadia kutatua changamoto ya baadhi ya taasisi za umma kutofanyia kazi taarifa ambazo wamekuwa wakizitoa kwa lengo la kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa haki za binadamu nchini. 

“Mhe. Waziri, tunaomba tuwe tunakupatia nakala ya taarifa za masuala ya utawala bora ambazo huwa tunaziandaa ili kwa mamlaka yako utusaidie kukemea taasisi ambazo zimekuwa hazishughulikii ipasavyo taarifa ambazo tumekuwa tukizitoa kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na kusimamia misingi ya utawala bora,” Mhe Jaji Mstaafu Mwaimu amefafanua. 

Mhe. Mwaimu ameongeza kuwa, licha ya Tume anayoingoza kuwa na jukumu la kushughulikia suala la kukuza na kuimarisha haki za binadamu, Tume yake pia ina jukumu la kuisaidia Serikali kulinda haki za wananchi na kusimamia vema misingi ya utawala bora, hivyo Tume yake itaendelea kuwa jicho pekee la kubaini changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haki za binadamu ili Serikali ichukue hatua stahiki ya kuzitatua changamoto hizo. 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeitembelea Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira yake ya kuongoza ukuzaji, ulinzi na hifadhi ya haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu kwa ushirikiano na wadau. 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora waliofika ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi. Wengine ni watendaji wa Ofisi yake na wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (hawapo pichani) walipofika ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi. Kulia kakwe ni Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi yake Bw. Xavier Daudi. 


Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu akielezea majukumu ya tume yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama walipofika ofisini kwa Mhe. Jenista jijini Dodoma kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi.


Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu, Mhe. Nyanda Shuli akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa kikao kazi cha kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi kilichofanyika katika ofisi ya Mhe. Jenista Mhagama Mtumba jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, watendaji wa ofisi yake na wa tume hiyo waliofika ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kubadilishana uzoefu. Wa kwanza kulia kwake ni Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu na wa kwanza kushoto kwake ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiagana na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu mara baada ya kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kati ya Ofisi ya Mhe. Jenista na Tume hiyo.


 

No comments:

Post a Comment