Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 26 Februari, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka
Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na
Rasilimaliwatu katika halmashauri kutatua changamoto zinazokwamisha wananchi kupata huduma bora pindi
wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo jijini
Dodoma, wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na
Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa
kilichofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali
Mtumba.
Mhe. Ndejembi amesema, viongozi
hao wanapaswa kukerwa na changamoto zinazowakabili wananchi pindi wanapofuata
huduma katika maeneo yao ya kazi na kuchukua hatua stahiki ya kuwahimiza
watendaji wanaowasimamia kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Ndejembi amewahimiza
viongozi hao, ambao wengi wao wanatoka maeneo ya pembezoni kuhakikisha
wanasimamia vema rasilimaliwatu ili wananchi wapate huduma bora, kwani wananchi
wengi waishio pembezoni mwa nchi wanalazimika kutumia gharama kubwa kufuata
huduma kwenye ofisi za makao makuu ya mikoa na halmashauri za wilaya.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
viongozi hao kutatua changamoto zinazowakabili watumishi ili wasiwe na sababu
ya kutotoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza kuwa, anaamini viongozi hao
wanatambua wajibu wao katika kutatua kero za watumishi na wananchi kwa ujumla.
“Kuna changamoto ambazo mnahitaji
kuwasikiliza tu watumishi au wananchi na kutoa majibu sahihi, lakini mmekuwa na
tabia ya kukwepa jukumu hilo na kulielekeza kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI jambo
ambalo si sahihi kwani lipo ndani ya mamlaka zenu na uwezo wenu kiutendaji,”
Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara
ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bw. Steven Bavu
amesema watahakikisha wanatekeleza agizo la Mhe. Ndejembi la kutatua kero za
wananchi katika maeneo yao ya kazi.
Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala
na Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Bi. Judith Mahende amesema
Mhe. Ndejembi amewahimiza kutatua kero za wananchi kwasababu katika Serikali za
Mitaa ndio kuna wananchi wengi wanaowasilisha changamoto ili zitatuliwe, hivyo watatenga
muda wa kuwatembelea na kuwasikiliza ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Kikao kazi hicho kilicholenga kuhimiza
uwajibikaji kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala
na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilifunguliwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Anjela Kairuki na kufungwa na Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi kwa
niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu
wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati
akifunga kikao kazi cha viongozi hao jijini Dodoma kilicholenga kuboresha
utendaji kazi wao.
Sehemu
ya Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na
Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (hayupo pichani) wakati akifunga kikao kazi chao jijini Dodoma
kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
kufunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za
Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini
Dodoma kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Sekretarieti ya Mkoa
wa Singida, Bw. Pancras Kakwere ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao kazi cha
Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na
Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa akitoa neno la shukrani mara
baada ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga kikao kazi kikao kazi chao
kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.
Mkuu
wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Halmashauri ya Mji Handeni, Bw. Steven
Bavu akielezea namna watakavyotekeleza maelekezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
aliyoyatoa wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na
Wakuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu katika Serikali za Mitaa
kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.
Mkuu
wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Wilaya ya Rombo, Bi. Judith Mahende akiahidi
kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi aliyoyatoa wakati akfunga kikao
kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Utawala na
Rasilimaliwatu katika Serikali za Mitaa kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.
No comments:
Post a Comment