Wednesday, February 22, 2023

TASAF YAELEKEZWA KUJENGA WODI YA AKINA MAMA NA AKINA BABA KATIKA ZAHANATI YA LUSHAMBA ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA

Na. James K. Mwanamyoto-Sengerema

Tarehe 22 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameulekeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga wodi ya akina mama na akina baba kufuatia maombi ya wananchi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakipata adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Zahanati ya Lushamba inayoboreshwa na TASAF mkoani Mwanza.

Mhe. Jenista amesema, kwa heshima ya wananchi wa Kijiji cha Lushamba, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TASAF itajenga wodi hizo mbili ya akina mama na akina baba mara baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Lushamba na miundombinu yake.

“Baada ya awamu ya pili ya ujenzi wa miradi ya Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC) kukamilika, TASAF hakikisheni mnajenga wodi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanawake na wanaume watakaohitajika kulazwa katika zahanati hiyo ya Lushamba,” Mhe. Jenista amesisitiza

Ameongeza kuwa, fedha hizo za miradi ya OPEC zimepatikana kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihangaikia maendeleo ya nchi yake, hivyo ni vema kumuunga mkono katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Akizungumzia adha wanayoipata wananchi wa Kijiji cha Lushamba katika kupata matibabu, Mhe. Jenista ameelekeza kukamilika haraka kwa Kituo cha Afya cha Lushamba ifikapo tarehe 31 Machi, 2023.

Ameongeza kuwa zahanati hiyo ikikamilika itawawezesha akina mama kupata huduma salama ya afya ya uzazi kwani watoto watakaozaliwa ni rasilimali muhimu itakayotoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia adha ya huduma ya afya wanayoipata, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Lushamba, Bi. Monica Pawenzu amesema wamekuwa wakihangaika sana kupata huduma ya afya ya uzazi kwa kuingia gharama ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Bi. Pawenzu amemshukuru Mhe. Jenista kwa kuelekeza ukamilishaji wa zahanati pamoja na ujenzi wa wodi mbili ya akina mama na akina baba kwani itawawezesha kupata huduma za afya za uhakika na kwa gharama nafuu.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji Lushamba, Kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo mkoani Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza hoja ya mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Lushamba, Kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa, wilayani Sengerema alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo mkoani Mwanza


Mwonekano wa Kituo cha Afya, kinachoendelea kujengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kijiji cha Lushamba, Kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwahimiza viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kukamilisha mradi wa ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Chema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwasisitiza wanafunzi wa Shule ya Msingi Chema, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kusoma kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za serikali za kujenga madarasa katika shule hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akihimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

 

No comments:

Post a Comment