Friday, February 24, 2023

MHE. NDEJEMBI AWAHIMIZA VIONGOZI NA WATENDAJI MIKOANI KUIUNGA MKONO SERIKALI KWA KUBUNI MBINU MBALIMBALI ZITAKAZOWAWEZESHA WALENGWA WA TASAF KUJIINUA KIUCHUMI

 Na. Veronica Mwafisi-Makambako

Tarehe 24 Februari, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza Viongozi na Watendaji mikoani kuiunga mkono Serikali kwa kubuni mbinu mbalimbali zitakazowawezesha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kujiinua kiuchumi.

Mhe. Ndejembi amesema hayo wakati wa ziara yake yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

Mhe. Ndejembi amewahimiza viongozi na watendaji hao kufuatia Uongozi wa Mkoa wa Njombe ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka kubuni mbinu ya utekelezaji wa kilimo cha upandaji parachichi kwa kuwapatia miche ya parachichi walengwa hao ili kujiendeleza kimaisha.

Mhe. Ndejembi amesema kuwa, lengo la mradi wa TASAF ni kumuinua mwananchi kutoka kwenye hali duni ya maisha na kumfikisha katika hatua nyingine ya juu, hivyo ni vizuri mwananchi huyo akasaidiwa kwa kufanya shughuli za maendeleo ili aweze kujitegemea kiuchumi.

“Nina hakika kwa kupanda miche hii ya parachichi, kaya hizi za walengwa wa TASAF zitainuka kwa kujiongezea kipato na kumuwezesha mlengwa kuishi maisha bora,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa walengwa hao wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako kutoa ushirikiano katika kutekeleza kilimo cha parachichi kwani kinalenga kuwanufaisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka amesema, Mkoa wa Njombe unafaidika na kilimo cha parachichi kwani ndani ya miaka mitatu mkulima anaweza kuvuna, hivyo waliona wawasaidie walengwa wa TASAF kuwaandalia mazingira mazuri ya kujishughulisha na kilimo cha parachichi kwa lengo la kuwaongezea kipato.

Mhe. Mtaka amesema hayo yote yanatekelezwa kwa walengwa wa TASAF kwa lengo la kupunguza tatizo la umaskini nchini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Njombe iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hiyo mkoani Njombe.


Baadhi ya wananchi na walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hiyo mkoani Njombe.


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe. 


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Augustino Ngude akitoa salamu za TASAF kwa wananchi na walengwa wa TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo mara baada ya kukabidhi miche kwa walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hiyo mkoani Njombe.


Mwonekano wa miche ya parachichi waliyopatiwa walengwa wa TASAF katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

 



No comments:

Post a Comment