Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 19 Februari, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA) kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa karakana ya ndege (Hangar) kwa ajili ya matengenezo na usalama wa ndege za viongozi, ikiwa ni pamoja na kujipanga kwa ujenzi wa makao makuu ya ofisi na karakana ya ndege jijini Dodoma.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA) chenye lengo la kiuhimiza uwajibikaji kwa watendajii wa wakala hiyo.
Mhe. Jenista amesema pamoja na kuitaka TGFA kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa karakana ya ndege jijini Dar es Salaam kwa wakati, kuna haja ya kujenga karakana nyingine jijini Dodoma ambapo ujenzi huo unapaswa kwenda sambamba na ujenzi wa ofisi ya TGFA makao makuu jijini humo.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, ujenzi wa ofisi ya Wakala ya Ndege za Serikali na karakana ya ndege jijini Dodoma unalenga kuunga mkono nia na azma ya Serikali ya kuhamia Dodoma, hivyo ameisitiza menejimenti ya wakala hiyo kuhakikisha inafanya jitihada za kuanza ujenzi haraka iwezekanavyo.
“Tuna kila sababu kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuomba fedha za ujenzi wa karakana ya ndege na makao makuu ya ofisi ya TGFA jijini Dodoma kwa lengo la kuongeza ufanisi kiutendaji na kuunga mkono azma ya Serikali ya kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mradi wa ujenzi wa karakana ya ndege jijini Dar es Salaam ni mradi pekee unaotekelezwa na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambao ujenzi wake ukikamilika kwa wakati utaiwezesha wakala kupata sehemu salama ya kufanyia matengenezo ya ndege zinazotumika kuwahudumia viongozi wakuu wa kitaifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Menejimenti ya Wakala ya Ndege za Serikali wakati wa kikao kazi chake na menejimenti hiyo jijini Dar es Salaam kilicholenga kuhimiza uwajibikaji. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais-Ikulu, Bibi Ened Munthali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwenye Menejimenti ya Wakala ya Ndege za Serikali wakati wa kikao kazi chake na menejimenti hiyo jijini Dar es Salaam kilicholenga kuhimiza uwajibikaji. Kushoto kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais-Ikulu, Bibi Ened Munthali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiongoza kikao kazi chake na Menejimenti ya Wakala ya Ndege za Serikali jijini Dar es Salaam kilicholenga kuhimiza uwajibikaji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule akifafanua jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Menejimenti ya Wakala ya Ndege za Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wakala ya Ndege za Serikali wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Wakala hiyo kilichofanyika jijini Da es Salaam kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment