Wednesday, February 22, 2023

NYARAKA ZINAZOHIFADHIWA KATIKA KITUO CHA KUMBUKUMBU KANDA YA ZIWA ZINARAHISISHA UTENDAJI KAZI WA SHUGHULI ZA SERIKALI KATIKA KANDA HIYO-Mhe. Jenista

Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza

Tarehe 22 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema kumbukumbu na nyaraka zinazohifadhiwa katika Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa zinarahisisha utendaji kazi wa shughuli za serikali za kila siku kwenye maeneo ya Kanda hiyo.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Mwanza wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa kituo hicho pamoja na viongozi na watendaji wa serikali kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kituo hicho.

Mhe. Jenista amesema nyaraka ni uti wa mgongo wa utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa kuwa maamuzi yote yanayofanywa na serikali yanategemea kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa kwa ajili ya rejea ya kiofisi.

Akifafanua zaidi kuhusiana na nyaraka zilizohifadhiwa katika kituo hicho cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa, Mhe, Jenista amesema, ameshuhudia baadhi ya kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa ambazo zinaeleza historia ya taifa letu kabla ya uhuru, wakati wa uhuru na baada ya uhuru na kuongeza kuwa nyaraka hizo ni urithi wa taifa letu.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, nyaraka hizo pia ni muhimu katika kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi ambayo ipo na inaendelea kujitokeza katika jamii kwani zinaonyesha uthibitisho wa mipaka na uhalali wa umiliki wa ardhi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi amesema kumbukumbu zinazohifadhiwa katika kituo hicho hupatikana kwa urahisi zinapohitajika kwa ajili ya rejea mbalimbali. 

Bw. Msiangi ametoa mfano wa majalada ya mashauri ya Mahakama ya Tanzania yaliyofungwa na kuhifadhiwa katika kituo hicho kuhitajika mara kwa mara kwa ajili ya rejea ya maamuzi ya mashauri mbalimbali na rufaa zinazowasilishwa kwenye mamlaka husika. 

Katika kuongeza ufanisi wa kiutendaji, Bw. Msiangi amesema kituo hicho kitaunganishwa na mfumo wa serikali mtandao ili kuwezesha nyaraka zitakazohifadhiwa kituoni kuwa katika mfumo wa kidijitali kwa lengo la kulinda nakala halisi na kurahisisha upatikanaji wake pindi zinapohitajika.

Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kimekuwa msaada mkubwa kwa rejea ya kiofisi na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za serikali katika Kanda ya Ziwa. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akionyeshwa moja ya nyaraka zilizoko katika Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichoko jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kituo hicho. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali jijini Mwanza (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa watumishi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.  


Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi, akitoa maelezo ya awali kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kuhusu Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo jijini Mwanza wakati wa ziara ya kikazo ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kituo hicho.


 

No comments:

Post a Comment