Tuesday, February 7, 2023

KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 07 Februari, 2023

Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Machano Saidi amesema ili kuboresha utunzaji wa kumbukummbu na nyaraka Zanzibar, kamati yake imefanya ziara ya kikazi katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa lengo la kujifunza namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa.

Mhe. Saidi amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha kamati yake na Viongozi na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kilicholenga kubadilisha uzoefu wa utendaji kazi.

Mhe. Saidi amefafanua kuwa, kutokana na historia ya Zanzibar, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka ni jambo linalopewa kipaumbele na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio maana kamati yake imefanya ziara yenye lengo la kujifunza utunzaji mzuri wa kumbukumbu na nyaraka ili taifa liendelee kuwa historia yenye tija kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Akizungumzia ziara ya kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na  Utawala Bora, Mhe Jenista Mhagama amesema anatambua kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mdau muhimu sana katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo ujio wa kamati hiyo utatoa fursa ya kubadilishana uzoefu katika eneo la utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar watapata fursa ya kujifunza kuhusu namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa kutumia mifumo ya kidijitari inayotumiwa na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kutunza kumbukumbu na nyaraka na kuwezesha watendaji wa Serikali kuzitumia kwa rejea ya kiofisi.

“Nina hakika waheshimiwa wajumbe wa kamati mtajionea mifumo ya TEHAMA inayotumika kuhifadhi na kutumia kumbukumbu na nyaraka za taifa pia mtajionea namna zinavyoandaliwa ili kuhifadhiwa, ikiwa ni pamoja na kuona vifaa vinavyotumika kuandaa na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka hizo, ” Mhe. Jenista amefafanua.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Ikulu - Zanzibar, Mhe. Jamal Ali amesema kuwa ofisi yake iliratibu ziara ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ili kuiwezesha kamati hiyo kutimiza lengo la kujifunza na hatimaye kushauri namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa Idara ya Kumbukumbu ya Zanzibar.

Akieleza majukumu yanayotekelezwa na Idara yake ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Mkurugenzi wa Idara hiyo Bw. Firimin Msiangi amesema miongoni mwa majukumu yanayotekelezwa na idara yake ni kukusanya nyaraka zenye umuhimu kutoka katika taasisi za umma ili kulinda na kuhifadhi historia ya taifa.

Bw. Msiangi ameongeza kuwa, idara yake ina jukumu la kuweka mifumo ya kidijitari ya utunzaji kumbukumbu katika taasisi za umma ili kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma Serikali na kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi nyaraka zilizokusanywa kutoka katika taasisi za umma kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji wake zinapohitajika na kulinda nakala halisi.

Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamehitimisha ziara yao ya kikazi ya siku moja katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ambayo imewapa fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kiutendaji katika eneo la utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa.

 

Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Viongozi na Watendaji wa Afisi ya Rais Ikulu Zanzibar na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mada kuhusu utunzaji wa nyaraka kupitia mifumo ya TEHAMA iliyokuwa ikiwasilishwa na Bw. Sigfrid Ngowi, Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Machano Saidi akiongoza kikao kazi cha kamati yake na Watendaji na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo kwenye Idara ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Machano Saidi (hayupo pichani) kuongoza kikao kazi cha kamati yake na Watendaji na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo kwenye Idara ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

 

 

Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Mhe. Jamal Ali akielezea matarajio ya SMZ ya kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa kupitia uzoefu kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi (kushoto) na Katibu Mkuu, Afisi ya Rais Ikulu - Zanzibar Bw. Salehe Juma Mussa (kulia) wakifuatilia mada juu ya utunzaji wa nyaraka kupitia TEHAMA iliyowasilishwa Bw. Sigfrid Ngowi, Afisa Tehama Mwandamizi (hayupo pichani) kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi akielezea majukumu ya taasisi yake kwa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

 

 

Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango akielezea namna TEHAMA inavyorahisisha utendaji kazi katika shughuli za Serikali wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


 

Bw. Sigfrid Ngowi, Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa akiwasilisha mada juu ya utunzaji wa nyaraka kupitia TEHAMA kwa Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Machano Saidi akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati yake pamoja na Viongozi na Watendaji wa Afisi ya Rais Ikulu Zanzibar na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo kwenye Idara ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

 

 

 

No comments:

Post a Comment