Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 12 Februari, 2023
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Jenista Mhagama, amesema watumishi wa ofisi yake wametoa msaada wa mahitaji
mbalimbali kwa wenye uhitaji katika Kituo cha Matumaini Mihuji na Nyumba ya
Amani na Furaha Hombolo inayotunza wazee na watoto ili kujenga matumaini ya
wahitaji hao na kuwawezesha kutimiza ndoto za maisha yao.
Mhe. Jenista
amesema hayo wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa wenye uhitaji
katika kituo cha matumaini Mihuji jijini Dodoma.
Mhe. Jenista
amesema, msaada walioutoa unaunga mkono malezi kwa wenye uhitaji kwani
wanaamini kuwa watoto wenye uhitaji ndio watumishi wa umma na viongozi wa
baadae, hivyo msaada huo ni sehemu ya kuchangia ujenzi wa msingi mzuri wa
watoto hao kuwa watumishi wa umma na viongozi wa baadae watakaotoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Mhe. Jenista
ameongeza kuwa, jamii isipowasaidia wenye uhitaji watakosa mwelekeo na hapo
baadae hakutakuwa na rasilimaliwatu itakayotekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya
Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE ambayo inajenga
ari ya kila mtanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa pamoja na kuandaa
rasilimaliwatu itakayokuwa na tija katika utoaji huduma kwa wananchi.
Aidha, Mhe.
Jenista amesema, msaada wa vitu uliotolewa na watumishi wa ofisi yake katika
Kituo cha Matumaini Mihuji na Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo imetokana na
michango binafsi ya watumishi na si fedha ya Serikali.
“Michango
iliyokusanywa imetuwezesha watumishi wote kuacha familia zetu na kuja kuwafariji
wenye uhitaji, niwahakishie hakuna mtumishi yeyote aliyesalia nyumbani kwake
wakati wa zoezi hili muhimu la kutoa faraja kwa wahitaji,” Mhe. Jenista
amefafanua.
Akikabidhi
msaada kwenye Nyumba ya Amani na Furaha inayotunza wazee na watoto Hombolo,
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Deogratius Ndejembi amesema msaada alioukabidhi kwa niaba ya watumishi wa
ofisi yake japokuwa ni mdogo lakini ni sadaka inayojitosheleza na kuongeza kuwa,
watumishi wameguswa kwasababu wanathamini mchango wa wazee ambao wakati wakilitumikia
taifa walijituma kwa moyo na uzalendo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza
kwa niaba ya uongozi wa Kituo cha Matumaini Mihuji, Sista Elizabeth John amewashukuru
watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuwatembelea na kutoa msaada
utakaosaidia malezi ya watoto katika kituo chao na kuahidi kuwa misaada hiyo
itatumika kama ilivyokusudiwa.
Mmoja wa
watoto anayelelewa katika Kituo cha Matumaini Mihuji Bi. Elizabeth Francis,
amemshukuru Mhe. Jenista na watumishi wa ofisi yake kwa msaada walioutoa na
kuahidi kuendelea kuwaombea ili waweze kutekeleza vema majukumu yao ya
kulitumikia taifa.
Naye,
Msaidizi wa Kituo cha Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo Sista Maria Radiance
amesema, sadaka iliyotolewa na watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kituo
chao itasaidia malezi ya wazee na watoto kituoni hapo na kuongeza kuwa ujio wa
watumishi hao ni tendo la upendo ambalo linatokana na msukumo wa Mwenyezi
Mungu.
Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeshiriki shughuli za kijamii kwa lengo la
kujenga mahusiano mazuri na jamii yatakayokuwa na tija katika kupata mrejesho utakaoboresha
huduma katika Utumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watoto wenye uhitaji
alipowatembelea katika kituo cha Matumaini Mihuji jijini Dodoma kwa lengo la kutoa
msaada wa kijamii katika kituo hicho.
Sehemu ya watoto wenye uhitaji katika Kituo cha Matumaini
Mihuji wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza nao kwenye kituo
hicho jijini Dodoma kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na Uongozi wa Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo jijini
Dodoma inayotunza wazee na watoto alipokitembelea kituo hicho kwa lengo la
kutoa msaada wa kijamii. Katikati aliyekaa ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi mafuta ya kupikia ikiwa
ni sehemu ya msaada uliotolewa na watumishi
wa ofisi yake katika kituo cha Matumaini Mihuji jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhi kiroba cha
unga ikiwa ni sehemu ya msaada uliotolewa
na watumishi wa ofisi yake katika Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo inayotunza wazee
na watoto. Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimpatia zawadi mmoja wa watoto
wanaolelewa katika kituo cha Matumaini Mihuji jijini Dodoma alipokitembelea kituo
hicho kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akiwapatia zawadi watoto wanaolelewa
katika Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo alipokitemebela kituo hicho kwa lengo la kutoa msaada wa mahitaji ya vitu
mbalimbali jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kuwasalimia
wazee na watoto wanaotunzwa katika
Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii katika
kituo hicho. Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro pamoja na
watendaji wengine wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Aliyekaa na watoto chini) akiwa
katika picha ya pamoja na watoto wanaolelewa katika kituo cha Matumaini Mihuji
alipokitembelea kituo hicho kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii.
No comments:
Post a Comment