Sunday, February 5, 2023

FURSA ZA MAFUNZO KWA WATANZANIA NJE YA NCHI NI MATOKEO YA MAHUSIANO MAZURI YA KIDIPLOMASIA YANAYOJENGWA NA RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 05 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema fursa za mafunzo kwa Watanzania zinazopatikana nje ya nchi zikiwemo za watumishi wa umma ni matokeo ya mahusiano mazuri ya kidiplomasia na wadau wa maendeleo yanayojengwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na watumishi wa umma walionufaika wa mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA). 

Mhe. Jenista amesema, kumekuwa na ongezeko la fursa za mafunzo ya muda mrefu na mfupi nchini Korea, China na India ambazo ni matunda ya kazi nzuri ya kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na wadau mbalimbali wa maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. 

Akizungumzia umuhimu wa fursa hizo za mafunzo, Mhe. Jenista amesema Serikali itazitumia ipasavyo kuendeleza rasilimaliwatu iliyopo ile iendane na kasi ya maendeleo ya teknolojia, ambayo hivi sasa ina nafasi kubwa ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma. 

“Watakaonufaika na fursa hizi za mafunzo, ndio watakaolisaidia taifa kuendana na kasi ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na hata ukiwasikiliza vizuri wanufaika hawa utabaini kuna maarifa ya ziada waliyoyapata ambayo yatawasaidia kuongeza ufanisi kiutendaji,” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Mhe. Jenista amefafanua kuwa, nchi ya Korea ina utamaduni mzuri wa ufanyaji kazi katika Utumishi wa Umma, hivyo waliobahatika kupata mafunzo nchini humo watakuwa ni chachu ya kuboresha utendaji kazi nchini na kuondokana na ufanyaji kazi wa mazoea wa baadhi ya watumishi wa umma, na kuongeza kuwa fursa za mafunzo zikiongezeka na wanufaika wakitumika vizuri ni dhahiri kuwa taifa litapiga hatua kimaendeleo.  

Mmoja wa watumishi walionufaika na mafunzo nchini Korea kupitia ufadhili wa KOICA, Bw. Tamko Ngumbuke ambaye ni Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, amesema alifanya utafiti katika eneo la masoko ya mazao ya kilimo na kubaini kuwa, kukiwa na vyama vya ushirika imara ambavyo vitakuwa na ushirikiano na taasisi za kiteknolojia na zinazofanya tafiti katika masuala ya kilimo zitawazesha wakulima kupata masoko ya uhakika ambayo watayatumia kuuza mazao yao na kuona faida ya kilimo. 

Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao waliosoma Korea, Bw. Juma Mkabakuli amesema, ana imani kuwa watumishi wote walionufaika na mafunzo hayo watakuwa na mchango katika taifa kulingana na maeneo ya kitaaluma waliyosomea. 

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imekuwa ikiratibu fursa za mafunzo zinazotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo kwa kipindi hiki cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita, idadi ya Watanzania wanaonufaika na fursa hizo imeongezeka.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa umma walionufaika na mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA) mara baada ya watumishi hao kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi yake, Bw. Xavier Daudi na wa pili ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Dkt. Edith Rwiza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Bw. Juma Mkabakuli wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambaye ni mmoja wa watumishi wa umma walionufaika na mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA) mara baada ya watumishi hao kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. 


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na watumishi wa umma walionufaika na mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA) mara baada ya watumishi hao kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. 


Mmoja wa watumishi wa umma walionufaika na mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA) Bi. Maria Nkangali ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Kibaha akielezea namna alivyonufaika na mafunzo mara baada ya watumishi hao kumtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ofisini kwake jijini Dodoma. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa umma walionufaika na mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA) mara baada ya watumishi hao kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. Wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi

 


 

No comments:

Post a Comment