Tarehe 25 Januari,
2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa
wito kwa wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, kurasimisha ardhi ili kupata mtaji
wa kujenga nyumba za wageni za kawaida zinazohitajika na watalii wengi wanaotembelea
Kiwengwa Wilaya ya Unguja Kaskazini B kwa ajili ya kufanya utalii.
Mhe. Jenista ametoa wito huo wakati
wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa Kituo Jumuishi cha
Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara, kilichojengwa na Mpango wa Kurasimisha
Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A.
Mhe. Jenista amesema, amelazimika kutoa wito huo kwa wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwasababu alipotembelea eneo la Kiwengwa alishuhudia watalii wakihitaji zaidi nyumba za wageni za kawaida na kuongeza kuwa wananchi wakirasimisha ardhi watapata mtaji wa kujenga nyumba za wageni ili kujiongezea kipato.
“Niliona watalii wanapendelea zaidi kukaa kwenye nyumba za wageni zinazomilikiwa na wakazi wa Kiwengwa, hivyo ni wakati muafaka kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani kurasimisha ardhi ili kutumia fursa hiyo ya uwepo wa watalii,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha, Mhe. Jenista amesema wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wakirasimisha ardhi na biashara zao watasaidia kuongeza mapato ya Serikali ambayo yatatumika kuboresha miundombinu ya huduma kwa wananchi katika sekta afya, maji na barabara.
Mmoja wa wanufaika wa MKURABITA, Bw. Khamis Hussein amesema kuwa uwepo wa Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichopo Mkokotoni, kimemsaidia katika masuala mbalimbali ikiwemo kukopa fedha benki, kumuondolea adha ya kulazimika kwenda mjini ili kurasimisha biashara yake na pia amekuwa na uhakika wa usalama wa biashara yake, aidha, amewashukuru watendaji wa kituo hicho kwa kutoa huduma nzuri.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) CPA Dkt. Seraphia Mgembe amesema ushuhuda wa namna Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilivyowawezesha wajasiliamali kuokoa muda wa kufuata huduma ya urasimishaji mjini na kuwawezesha kukopa kwenye taasisi za kifedha ili kupata mtaji, ndio lengo kuu la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
CPA Dkt. Seraphia Mgembe amesisitiza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja kupitia MKURABITA zimedhamiria kumuwekea mazingira mazuri ya ujasiriamali Mtanzania anayefanya shughuli za kiuchumi ili kutekeleza jukumu lake bila wasiwasi au hofu yoyote ya kupoteza muda wake au rasilimali fedha.
Sehemu ya wajasiriamali na wafanyabiashara wa Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuzindua Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara, Zanzibar.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo ya Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichojengwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) eneo la Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Ameir
akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza
na wajasiriamali na wafanyabiashara wa Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa
wa Kaskazini Unguja wakati wa uzinduzi wa Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na
Uendelezaji wa Biashara, Zanzibar.
Mkuu
wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Ayoub Mahmoud akitoa salamu za mkoa wake
kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wajasiriamali na
wafanyabiashara wa Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja
wakati wa uzinduzi wa Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa
Biashara, Zanzibar.
Mratibu
wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania
(MKURABITA), CPA. Dkt. Seraphia Mgembe akielezea majukumu ya taasisi yake kabla
ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na
Uendelezaji wa Biashara kilichopo eneo la Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A,
Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.
Mmoja wa
wanufaika wa MKURABITA, Bw. Khamis Hussein akieleza namna alivyonufaika na
Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara cha Mkokotoni,
Wilaya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.
No comments:
Post a Comment