Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 21 Februari,
2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, watumishi wa ofisi yake wanao wajibu wa kumsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kujenga na kusimamia vema rasilimaliwatu katika sekta zote ili rasilimaliwatu hiyo itumike kuleta maendeleo endelevu.
Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma katika siku maalum (UTUMISHI DAY GALA 2022), iliyoandaliwa na menejimenti ya ofisi yake kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi kwa watumishi wa ofisi yake.
Waziri Jenista amesema, juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais kujenga rasilimaliwatu katika sekta za elimu, afya, kilimo, madini, maji, nishati, anga na miundombinu ya barabara na reli zinapaswa kuungwa mkono kwa vitendo na watumishi wote wa umma nchini ili kuchangia ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
“Wajibu wetu sisi ni kumsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha rasilimaliwatu Serikalini ili sekta zote zitoe mchango chanya katika ujenzi wa uchumi imara na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ametoa wito kwa watumishi wa ofisi yake, kujenga umoja na mshikamano ili kuweka mazingira rahisi na rafiki ya utendaji kazi ambao utakuwa unaunga mkono kwa vitendo jitihada za Mhe. Rais za kutoa huduma bora kwa wananchi na kuleta maendeleo kwa taifa.
“Tupendane na tuishi kama ndugu kwani mafanikio ya kila mmoja wetu ni mafanikio ya ofisi yetu na utumishi wa umma kwa ujumla, tuna kila sababu ya kufanya kazi kwa bidii, weledi, uzalendo na kwa kuzingatia miiko, Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi ikiwa ni pamoja Sheria,Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma iliyopo kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa letu,” Mhe. Jenista amefafanua.
Aidha, amewataka watumishi wa ofisi yake kuwa ni kioo na mfano bora wa kuigwa kiutendaji na watumishi wa taasisi zote za umma nchini, kwani ofisi yake ndio imepewa jukumu kubwa la kumsaidia Mhe. Rais kusimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amesema watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI ndio wamebeba dhamana ya maisha ya watumishi wote wa umma na ustawi wao hivyo amewataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii.
Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amewapongeza kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kutoa mchango katika sekta ya utumishi wa umma na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amewashukuru watumishi wa ofisi yake kwa kufanya kazi kwa bidii katika mwaka uliopita wa 2021 na kuwakumbusha kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutoa huduma bora.
Siku Maalum ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (UTUMISHI DAY GALA 2022) iliyoandaliwa kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi, imetumiwa na watumishi wa ofisi hiyo kujitathmini kiutendaji ili kuendana na kasi ya utendaji kazi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Kaulimbiu yake ya KAZI IENDELEE.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa ofisi yake katika ukumbi wa Vijana jijini Dodoma, mara baada ya watumishi hao kumpatia tuzo ya kumtambua kuwa ni kiongozi bora wa kuigwa na Watumishi wa Umma katika siku maalum (UTUMISHI DAY GALA 2022) iliyoandaliwa kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa ofisi yake jijini Dodoma katika siku maalum (UTUMISHI DAY GALA 2022), iliyoandaliwa na menejimenti ya ofisi yake kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi kwa watumishi wa ofisi yake.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akimpatia zawadi ya utendaji kazi mzuri Katibu Mahsusi Bi. Joyce Chitalula katika siku maalum (UTUMISHI DAY GALA 2022), iliyoandaliwa na menejimenti ya ofisi yake kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi kwa watumishi wa ofisi yake.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi akimpatia zawadi Katibu Mahsusi Bi. Maria Rutatina kwa kuzingatia muda wa kuwasili katika siku maalum (UTUMISHI DAY GALA 2022), iliyoandaliwa kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi kwa watumishi wa ofisi yake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimpatia zawadi ya utumishi wa muda mrefu Katibu Mahsusi Bi. Salma Nahoda, katika siku maalum (UTUMISHI DAY GALA 2022) iliyoandaliwa na ofisi yake kwa lengo la kujenga umoja na kuongeza chachu ya utendaji kazi.
No comments:
Post a Comment