Thursday, February 3, 2022

SERIKALI YAJA NA MFUMO WA KIELEKTRONIKI KUTATUA CHANGAMOTO YA UPUNGUFU WA WATUMISHI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 03 Februari, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amesema, Ofisi yake imebuni Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Hali ya Rasilimaliwatu utakaoiwezesha  Serikali kupata taarifa sahihi kuhusu idadi na mgawanyo wa watumishi katika Taasisi za Umma kwa lengo la kutatua changomoto ya upungufu wa watumishi unaoathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ameeleza hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali akiwa ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma.

“Uzoefu unaonyesha kuwa, baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikiwasilisha maombi ya mahitaji ya watumishi bila ya kufanya uchambuzi wa kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya watumishi. Hali hii inasababisha baadhi ya Taasisi za Umma kuwa na Watumishi wengi kuliko mahitaji yao halisi au Watumishi wachache kuliko inavyohitajika,” Mhe Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, hali hiyo inasababisha watumishi kurundikana katika kituo kimoja kuliko mahitaji wakati vituo vingine vina watumishi wachache au kukosa kabisa watumishi hivyo kuathiri utendaji kazi na utoaji huduma kwa umma.

Akizungumzia faida za mfumo huo, amesema utasaidia kuainisha na kuandaa mahitaji halisi ya watumishi kwenye Taasisi zote za Umma na kuongeza kuwa, kwa kufanya hivyo Serikali itakuwa na taarifa na takwimu sahihi kuhusu mahitaji ya watumishi waliopo na wanaohitajika.

Aidha, Mhe. Jenista  amewataka Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma nchini kusimamia utekelezaji wa zoezi la kubaini mahitaji halisi ya watumishi katika Taasisi za Umma ambalo litafanyika kuanzia mwezi huu wa Februari 2022.

“Tekelezeni zoezi hili la kubaini mahitaji halisi ya watumishi bila kuwabughudhi Watumishi wa Umma na huku mkitambua kuwa Serikali imewekeza rasilimali fedha ya kutosha,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Lengo la Serikali kuanzisha Mfumo wa Kielektoniki wa Tathmini ya Hali ya Rasilimawatu ni kukusanya taarifa za Taasisi, watumishi na huduma zinatolewa na taasisi za umma ili zitumike kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali kwa wananchi. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumzia namna Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Hali ya Rasilimaliwatu utakavyoiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi kuhusu idadi na mgawanyo wa watumishi katika Taasisi za Umma.

No comments:

Post a Comment