Friday, February 18, 2022

MHE. JENISTA AITAKA TPA KUWA NA UBUNIFU WA KUONGEZA MAPATO YATAKAYOIWEZESHA SERIKALI KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI

Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Tarehe 18 Februari, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwa na ubunifu kiutendaji ambao utaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato yatakayoiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ametoa wito huo kwa watumishi wa TPA, wakati akifungua kikao cha 31 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TPA kilichofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Magadu.

Mhe. Jenista amesema kuwa, mapato yatakayopatikana kupitia bandari yatatumiwa na Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta zote muhimu zinazotoa huduma ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja.

“Mapato ya bandari zetu ndio yataiwezesha Serikali kuboresha huduma za afya, elimu, barabara na umeme kwa Watanzania,” Mhe. Jenista amefafanua.

Waziri Jenista amawataka watumishi wa TPA kutambua kuwa, wana umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwani ubunifu na nguvu kazi yao ina mchango mkubwa wa maendeleo ya taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo hawana budi kufanya kazi kwa bidii ili taifa linufaike na utumishi wao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Eric Hamissi amesema, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, TPA imejiwekea malengo ya kukusanya shilingi trilioni moja ili kuiwezesha Serikali kutekeleza wajibu wake wa kuboresha huduma kwa wananchi.

“Itakapofika tarehe 30 Juni, 2022 tutakuwa tumekusanya shilingi trilioni moja, kwa mwendo tulionao nina imani tutafikia lengo kwani mpaka sasa ndani ya miezi saba, TPA imekusanya bilioni 610, hivyo kiasi cha shilingi bilioni 390 kilichobakia kitapatikana ndani ya miezi iliyobaki,” Bw. Hamissi amesisitiza.

Baraza hilo pamoja na mambo mengine limepokea na kujadili Taarifa ya Kamati ya Utendaji pamoja na Bajeti pendekezwa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wakati akifungua kikao cha 31 cha baraza hilo kilichofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Magadu.


Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kabla ya waziri huyo kufungua kikao cha 31 cha baraza hilo kilichofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Magadu.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Eric Hamissi akiwaonesha wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TPA kibali cha ajira alichotumiwa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI kupitia barua pepe yake, wakati kikao cha 31 cha baraza hilo kilichofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Magadu.


Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tannzania (DOWUTA) Bw. Jonathan Msoma akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, mara baada ya waziri huyo kufungua kikao cha 31 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TPA kilichofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Magadu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wakati akifungua kikao cha 31 cha baraza hilo kilichofanyika mjini Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Magadu.


 

No comments:

Post a Comment