Wednesday, February 9, 2022

TAKUKURU NI KIMBILIO LA WANYONGE DHIDI YA VITENDO VYA RUSHWA, DHURUMA, UBADHIRIFU NA HUJUMA - Mhe. Jenista

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 10 Februari, 2022


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amesema, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni kimbilio pekee la Watanzania wanyonge katika kuwaondolea tatizo la vitendo vya rushwa, dhuruma kwenye mirathi, hujuma zinazosababisha migogoro ya ardhi na ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi ya kimkakati ambazo zinazotokana na kodi za wananchi.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi  wa TAKUKURU akiwa kwenye ziara yake ya kwanza ya  kikazi kwenye taasisi hiyo, yenye lengo kujitambulisha  na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taaasisi hiyo.

“TAKUKURU ikitekeleza wajibu wake ipasavyo itaondoa vilio vya watu wengi ikiwemo wajane wanaodhurumiwa mirathi, Watanzania wanyonge wanaoingia kwenye migogoro ya ardhi kwa kudhurumiwa na wenye nacho, watoto wa kike wanaokabiliwa na changamoto ya vitendo vya rushwa mashuleni kutokana na jinsia yao ikiwa ni pamoja na kuondoa kilio cha watanzania na cha Mhe. Rais dhidi ya vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma zinazotolewa na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, katika kipindi cha uongozi wake  kiu yake kubwa ni kuona TAKUKURU ikitekeleza kwanza wajibu wa kuzuia vitendo vya rushwa kabla havijatokea katika jamii kwani gharama za kuzuia rushwa ni ndogo kuliko gharama za kupambana na vitendo vya rushwa.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329. Majukumu yanayotekelezwa na taasisi hiyo ni pamoja na kuelimisha umma kuhusu athari za rushwa, kuchunguza tuhuma za makosa ya rushwa, kuwafikisha watuhuniwa mbele ya vyombo vya sheria, na kuishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya mapambano dhidi ya rushwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jijini Dodoma na watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akizungumza nao jijini Dodoma alipofanya ziara yake ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU jijini Dodoma kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji katika taasisi hiyo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipokea nakala ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu 2017-2022 kwa ajili ya rejea yake kutoka kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo aliyoifanya katika ofisi za TAKUKURU jijini Dodoma yenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Mtumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Sabina Marijani akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama jijini Dodoma, wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo yenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza hoja ya Mtumishi wa TAKUKURU, Bi. Sabina Marijani (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo aliyoifanya ofisi ya TAKUKURU jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akilakiwa na Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mara baada ya Waziri huyo kuwasili katika Ofisi hizo jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

 

No comments:

Post a Comment