Na. Mary L.
Mwakapenda-Morogoro
Tarehe 10 Februari, 2022
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi ameazimia kufanya kikao na Watumishi Housing, TARURA, MORUWASA,
TANESCO na wakazi wa Kata ya Mkundi mkoani Morogoro wanaoishi kwenye nyumba za
Mradi wa Watumishi Housing ili kutatua changamoto ya miundombinu iliyoharibiwa
na mvua kwenye nyumba hizo za gharama nafuu zilizojengwa kwa ajili kuwapangisha
na kuwauzia Watumishi wa Umma na wanachama wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii.
Mhe.
Ndejembi amefanya uamuzi huo akiwa mkoani Morogoro baada ya kukagua Mradi wa nyumba
zilizojengwa na Watumishi Housing katika Kata ya Mkundi mjini Morogoro na kukuta
miundombinu ya eneo hilo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea
kunyesha mkoani humo.
Naibu
Waziri Ndejembi amesema atafanya kikao hicho siku ya Jumamosi ya tarehe 19
Februari, 2022 ili kuwawezesha wakazi wengi wa eneo hilo ambao ni Watumishi wa
Umma kushiriki kikamilifu.
Akiwa
katika ukaguzi wa miundombinu ya eneo hilo, Mhe. Ndejembi amejionea madhara ya
mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo na kusababisha nyumba hizo kuingiliwa
na maji ya mvua ambayo imebomoa ukuta na mfereji wa kuzuia maji kuingia katika
makazi hayo na hatimaye kuharibu nyumba mbili pamoja na vitu vya ndani vya
nyumba hizo.
Mara
baada ya kumaliza ukaguzi wa maeneo yaliyoathirika na mvua zinazoendelea
kunyesha, Mhe. Ndejembi alikagua pia sehemu ambapo mkusanyiko wa maji unaanzia
na kuona kuna umuhimu wa kuzishirikisha taasisi nyingine na wananchi ili kuweza
kulimaliza kabisa tatizo hilo.
Ili
kukabiliana na athari zilizojitokeza kabla ya kufanyika kwa kikao rasmi cha
utatuzi wa tatizo la uharibifu wa miundombinu ya eneo hilo, Mhe. Ndejembi
amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa kuhakikisha
anachukua hatua za haraka za kuimarisha miundombinu ya ndani ya makazi hayo ambayo
imeharibika, ikiwa ni pamoja na kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine
katika kutafuta suluhu ya kudumu kabla ya kikao chake alichoelekeza kufanyika
Februari 19, 2022.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Dkt. Fred Msemwa ameahidi
kuyafanyia kazi maagizo ya Mhe. Ndejembi ili kuwawezesha wakazi wa eneo hilo
kuwa na miundombinu imara itakayohimiri changamoto ya mvua nyingi zinazoendelea
kunyesha katika eneo hilo.
Chanzo kikubwa cha kuharibika kwa miundombinu kwenye kata hiyo ya Mkundi mjini Morogoro ni barabara zinazozunguka eneo hilo kukosa mitaro ya maji hali inayopelekea mkondo wa maji kuelekea katika eneo la makazi ya watu.
Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akitoa maelekezo baada ya kukagua na kuona changamoto ya
miundombinu ya eneo la Mradi wa nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing
katika Kata ya Mkundi mjini Morogoro.
Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
akiangalia uharibifu wa miundombinu ya barabara uliosababishwa na mvua
zinazoendelea kunyesha kwenye eneo la Mradi wa nyumba zilizojengwa na
Watumishi Housing katika Kata ya Mkundi mjini Morogoro.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kukagua miundombinu ya eneo la Mradi wa nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing katika Kata ya Mkundi mjini Morogoro.
Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akiangalia uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua
zinazoendelea kunyesha kwenye Mradi wa nyumba zilizojengwa na Watumishi
Housing katika Kata ya Mkundi mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment