Wednesday, February 16, 2022

UTUMISHI YATEKELEZA MAELEKEZO YA MHE. RAIS KUUNDA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WANANCHI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 16 Februari, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, ofisi yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imetekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kusanifu Mfumo wa kielektroniki wa kupokea, kufuatilia na kushughulikia malalamiko (e-Mrejesho) ambao utatoa fursa kwa wananchi na wadau kuwasilisha malalamiko, maoni, mapendekezo, maulizo na pongezi Serikalini.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi (e-Mrejesho) yaliyotolewa kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Wakala na Idara Zinazojitegemea ambao wamepewa dhamana na taasisi zao kushughulikia malalamiko.

Mhe. Jenista amesema kuwa, mfumo huo wa kielektroniki uliosanifiwa na wataalam wazawa ni rafiki kwa wananchi na Watumishi wa Umma kuutumia, hivyo utakuwa ni mkombozi kwa Watanzania katika kuwasilisha malalamiko kwa wakati ili yafanyiwe kazi na Serikali.

“Ni mfumo ambao unatoa mrejesho kwa Watumishi wa Umma na wananchi kuhusu huduma zote zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia taasisi zake,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Sanjari na hilo, Mhe. Jenista amesema kuwa, licha ya mfumo huo kutoa taswira ya utendaji kazi wa Serikali, pia unatoa fursa kwa wananchi kutoa pongezi kwa Serikali, iwapo imefanya jambo jema lenye tija kwa taifa ili jambo hilo liendelezwe kwa manufaa ya umma.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inasisitiza sana ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa wakati katika taasisi zote za Umma, hivyo taasisi zote za umma zinapaswa kutoa kipaumbele cha kuutumia mfumo huo wa kielektroniki kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayowasiliswa katika taasisi zao.

“Mtakumbuka Hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa Mei, 2021 wakati akiwaapisha Mawaziri Waandamizi na Naibu Mawaziri alielekeza taasisi zote za umma nchini kuhakikisha zinatekeleza wajibu wa kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wakati, hivyo ni lazima agizo hili litekelezwe na taasisi zote za umma na ndio maana ofisi yangu imesanifu mfumo wa kieletroniki wa kushughulikia malalamiko ya wananchi,” Mhe. Jenista amefafanua.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na washiriki wa mafunzo, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema kuwa, amefarijika na kufurahi kuona wataalam waliotengeneza mfumo ni wazawa wa kitanzania ambao ni amali kwa taifa.

Bw. Daudi ameeleza kuwa, uundwaji wa mfumo huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais kwa vitendo yaliyolenga kuwa na Utumishi wa Umma wenye mtizamo chanya wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara yake ya Ukuzaji wa Maadili na Idara ya Mifumo ya TEHAMA imeandaa mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Kielektroniki wa kupokea, kufuatilia na kushughulikia malalamiko (e-Mrejesho) kwa Maafisa 100 wanaoratibu ushughulikiaji wa malalamiko katika taasisi za umma 50 zilizoko mkoani Dodoma.


 

Baadhi ya Maafisa Malalamiko na TEHAMA wakimsikiliza Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kabla ya kufungua rasmi mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko (e-Mrejesho) kwa maafisa hao yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Chuo cha VETA.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Mhe. Jenista Mhagama kufungua mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko (e-Mrejesho) kwa maafisa Malalamiko na TEHAMA yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Chuo cha VETA.

 

Mwenyekiti wa mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko (e-Mrejesho) Bw. Vicent Bukombe akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) mara baada ya Waziri huyo kufungua mafunzo hayo jijini Dodoma katika Ukumbi wa Chuo cha VETA.

 

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa ofisi yake na maafisa walioshiriki kutengeneza mfumo wa kielekroniki wa kupokea, kufuatilia na kushughulikia malalamiko (e-Mrejesho), mara baada ya Waziri huyo kufungua mafunzo ya Maafisa Malalamiko na TEHAMA waliopewa dhamana ya kuutumia mfumo huo.


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa ofisi yake na Maafisa Malalamiko na TEHAMA wanaohudhuria mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko (e-Mrejesho) mara baada ya Waziri huyo kufungua rasmi mafunzo hayo yanayofanyika kwa maafisa hao jijini Dodoma katika Ukumbi wa Chuo cha VETA.

 

No comments:

Post a Comment