Tuesday, March 21, 2023

WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WATAKIWA KUAINISHA NA KUZITAFUTIA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZITAKAZOKWAMISHA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2023/24

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 21 Machi, 2023

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la ofisi yake kuainisha na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zitakazokwamisha utekelezaji wa bajeti ya ofisi ya Mwaka wa Fedha 2023/24 inayotarajiwa kuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na Utawala Bora kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Bw. Mkomi ametoa maelekeo hayo jijini Dodoma, wakati akiongoza Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililofanyika kwa lengo la kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2022/23 na Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2023/24.

Bw. Mkomi amesema kila mwaka Bunge linaidhinisha bajeti lakini wakati wa tathmini mapungufu yanabainika katika utekelezaji, hivyo aliwasihi wajumbe wa baraza kutumia fursa ya mkutano huo kuainisha na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Ni wajibu wa kila mjumbe wa baraza hili kutoa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji wa bajeti yetu kwa mwaka wa fedha 2023/24 pindi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litakapoidhinisha” Bw. Mkomi amesisitiza.

Aidha, Bw. Mkomi amesema, ushirikiano wa kiutendaji chini ya uongozi wake ni suala analolipa kipaumbele ili kufikia azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi katika kutoa huduma bora.

Bw. Mkomi ametoa wito kwa wajumbe wa mkutano huo maalum kumshirikisha iwapo wana wazo au jambo ambalo wanafikiri likitekelezwa litakuwa na tija katika kuuboresha utumishi wa umma.

Bw. Mkomi ameongeza kuwa, suluhu ya kuboresha utendaji kazi wa watumishi wasiowajibika si kuwahamisha vituo vya kazi bali waajiri wahakikishe wanarekebisha mapungufu yao ili waendelee kutoa huduma katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa.

“Hata kwenye ofisi yetu, kama kuna mtumishi ana changamoto ya kutowajibika ipasavyo sitomuhamisha kwasababu itatafsiriwa kuwa nimempeleka mtu mwenye tatizo eneo lingine ili akaharibu, hivyo niwahakikishie kuwa mtumishi atakayehama ni yule mwenye utendaji mzuri ambaye atatoa mchango kiutendaji katika taasisi nyingine.” Bw. Mkomi ameongeza

Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2022/23 na Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2023/24, Mtakwimu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Ibrahim Kalengo amesema Serikali imeendelea kuunganisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi ili kubadilishana taarifa na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Bw. Kalengo ametolea mfano wa Mfumo Shirikishi wa Taarifa za kiutumishi na Mishahara kuunganishwa na Mfumo wa PSSSF, Mfumo wa Mikopo ya Elimu ya Juu, Mfumo wa Ajira Portal na Mfumo wa NIDA.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na kupitia Bajeti kwa Mwaka 2022/23 na Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2023/24 wamepata fursa ya kujadili na kuzitafutia suluhisho changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akiongoza Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) alipokuwa akiongoza Mkutano Maalum wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Musa Magufuli wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala pamoja na wajumbe wa Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala pamoja na wajumbe wa Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa katika mkutano maalumu wa baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cosmas Ngangaji akifafanua hoja kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Kamugisha Rufulenge akichangia hoja kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Mtakwimu Mkuu kutoka Idara ya Mipango Ofisi ya Rais-UTUMISHI akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na mapendekezo ya bajeti na mpango kazi wa mwaka wa fedha 2023/2024 kwenye Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mara baada ya kuhitimisha Mkutano Maalumu wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu wa Baraza la Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Rocky Setembo na kulia ni Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Kamugisha Rufulenge.


 

No comments:

Post a Comment