Na. James K. Mwanamyoto-Siha
Tarehe 3 Machi, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kila mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini anaishi maisha bora kama ambavyo Serikali imekusudia.
Mhe. Jenista amesema hayo akiwa katika Kijiji cha Wiri na Ngumbaru Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wakati akikagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.
Mhe. Jenista amesema, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliamua kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ili kuboresha maisha ya wananchi walio katika kaya maskini.
“Nimeenda kujionea mwenyewe namna walengwa wa TASAF walivyoanzisha miradi ya kufuga kuku, mbuzi na ng’ombe na wengine wamejenga nyumba za kuishi,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, uamuzi huo wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umewawezesha watoto wa walengwa wa TASAF kupata elimu bora na huduma bora za matibabu kupitia utekelezaji wa miradi ya elimu na afya ya TASAF na kuongeza kuwa, katika maeneo mengine walengwa wa TASAF wamefanikiwa kujiunga na bima ya afya inayowasaidia kupata huduma ya matibabu kwa urahisi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, amejionea mafanikio ya walengwa wa TASAF wilayani Siha na kuongeza kuwa pamoja na mafaniko hayo lakini bado Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea na jitihada zake za kutafuta fedha ili zitumike kuboresha maisha ya Watanzania wengi zaidi.
Mhe. Kikwete amewataka Watanzania kuendelea kuwa na imani na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha nia ya dhati ya kuboresha maisha ya wananchi anaowaongoza, hivyo walengwa wa TASAF hawana budi kumuunga mkono kwa kutumia vizuri ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao.
Naye, mmoja wa walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Ngumbaru wilayani Siha Bi. Kilei Kessy amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maisha yao kupitia ruzuku ya TASAF.
Bi. Kessy amesema, walengwa wa TASAF katika Kijiji chao wanaendelea vizuri, kwani kupitia TASAF wamepata uwezo wa kuwapeleka watoto wao shule, kujishughulisha na ufugaji pamoja na kujenga nyumba bora ambazo wanaishi na familia zao.
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeziwezesha kaya
maskini kupata huduma bora za afya, elimu na kuboresha maisha yao kwa kuongeza
kipato kupitia shughuli za ufugaji, kilimo na ujasiriamali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Wiri kata ya Gararagua Wilayani
Siha (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua
utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini wilayani humo.
Sehemu ya wananchi na walengwa wa
TASAF wa Kijiji cha Wiri Kata ya Gararagua Wilayani Siha wakimsikiliza Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo
iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini wilayani
humo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa
neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na
wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Wiri kata ya Gararagua Wilayani
Siha (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Jenista iliyolenga
kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini wilayani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete wakiwa kwenye zizi la ng’ombe la mlengwa wa TASAF Bi. Joyce
Kileo wa Kijiji cha Ngumbaru Kata ya Songu Wilayani Siha walipomtembelea
mlengwa huyo kushuhudia namna alivyoboresha maisha yake kupia TASAF.
Mwonekano wa nyumba iliyojengwa na
mlengwa wa TASAF Bi. Joyce Kileo wa Kijiji cha Ngumbaru Kata ya Songu Wilayani
Siha mkoani Kilimanjaro.
Mlengwa wa TASAF Bi. Kilei Kessy wa
Kijiji cha Ngumbaru, Kata ya Songu Wilayani Siha akitoa ushuhuda wa namna TASAF
ilivyoboresha maisha yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na
wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Ngumbaru kata ya Songu Wilayani
Siha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete wakiwa mbele ya nyumba ya mlengwa wa TASAF, Bi. Magdalena
Akaro wa Kijiji cha Ngumbaru Kata ya Songu Wilayani Siha walipomtembelea
mlengwa huyo kushuhudia namna alivyoboresha maisha yake kupia TASAF.
No comments:
Post a Comment