Saturday, February 10, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) YAIPONGEZA eGA KWA KULETA MABADILIKO KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi – Dodoma

Tarehe 10 Februari, 2024

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga na wajumbe wa kamati yake wameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kuleta mabadiliko katika utumishi wa umma kupitia Mifumo ya TEHAMA ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma bora nchini.

Mhe. Hasunga ameyasema hayo leo wakati kamati yake ilipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) ambacho kipo chini ya Mamlaka ya Serikali Mtandao.

“Kamati yetu imefurahishwa sana na utendaji kazi wa wataalam wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na taasisi yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA kwani haya yote tunayoyaona ni sehemu ya mabadiliko ya kuboresha utumishi wa umma nchini, kipindi cha nyuma haikuwa rahisi watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kupitia Mifumo ya TEHAMA,” Mhe. Hasunga amesema. 

Mhe. Hasunga ameipongeza eGA kwa jitihada kubwa inazofanya za kuunganisha mifumo ya TEHAMA iliyopo kwenye taasisi za umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati na mahali popote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Kituo kinafanya utafiti na kubuni mifumo ya TEHAMA Serikalini yenye uwezo kuongeza kasi katika jitihada za utoaji wa huduma kwa umma kwa haraka na gharama nafuu.

Mhe. Kikwete ameishukuru Kamati kwa kupanga ziara hiyo muhimu katika  kituo  ambapo ushauri na maelekezo yamepokelewa na Ofisi yake iko tayari kusimamia utekelezaji wake ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa teknolojia.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuisimamia Mamlaka ya Serikali Mtandao ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa wananchi kupitia Mifumo ya TEHAMA.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba ameishukuru kamati hiyo kwa kufanya ziara ya kikazi katika kituo hicho na kuahidi kuendelea kubuni mifumo mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na Viongozi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na watendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakati kamati hiyo ilipofanya ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma. 

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Eng. Benedict Ndomba (hayupo pichani) wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la utangulizi kwa   Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma. 


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la shukrani kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mara baada ya kuhitimisha ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Eng. Benedict Ndomba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) walipofanya ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.


Mjumbe wa Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe.  Emmanuel Ole Shangai akichangia hoja kuhusu serikali mtandao wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.

 






No comments:

Post a Comment