Na. James K. Mwanamyoto-Pwani
Tarehe 27 Julai, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma nchini kulipa deni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kutumia weledi wao kujenga uchumi wa taifa.
Akizungumza kwa
nyakati tofauti na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya
Wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Mhe.
Ndejembi amesema kuwa Mhe. Rais alipoingia madarakani, alitoa maelekezo kwa Waajiri
wote kuzingatia maslahi ya watumishi wa umma hususani suala la upandishwaji wa
madaraja jambo ambalo hivi sasa limetekelezwa na linaendelea kutekelezwa na
waajiri wote kikamilifu ikiwa ni pamoja na kulipa stahili za watumishi kwa
wakati.
Amesema waajiri
wote nchini wametekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, hivyo Watumishi wa Umma hawana
budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwani hakuna haki isiyokuwa na wajibu.
“Ni muda
mrefu tumekuwa tukililia haki ya kupandishwa madaraja na kupewa stahili
nyingine, Rais wetu ametusikia kwani wote waliostahili kupanda madaraja,
wamepanda na wenye madai ya stahili zao mbalimbali wamepatiwa, hivyo hili ni
deni na ili kulilipa deni hili tunapaswa kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii na
uadilifu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ameongeza
kuwa, Serikali itaendelea kujali maslahi ya Watumishi wa Umma kwasababu watumishi
ndio injini ya Serikali, hivyo wanalazimika kuendelea kutekeleza wajibu wao
ipasavyo.
Aidha, Mhe.
Ndejembi amezungumzia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika zoezi la upandishwaji
wa madaraja kwa Watumishi wa Umma kutokana na baadhi yao kukosa sifa kwa kutojaza
Fomu ya Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).
“Changamoto
ya upandishwaji madaraja kwa baadhi ya Watumishi ni kupuuza ujazaji wa OPRAS,
hawajazi kwa wakati na wanajaza kwasababu wanaona ni kigezo tu cha upandaji wa
madaraja.” Mhe. Ndejembi amefanua.
Ili kuongeza
ufanisi kiutendaji, Mhe. Ndejembi amewahimiza Watumishi wa umma nchini kufanya
kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Katika hatua
nyingine Mhe. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika kutoa elimu
kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaonufaika na Mradi wa kutoa
ajira za muda.
Amesema
suala la usimamizi wa walengwa wa TASAF ni la watumishi wote, hivyo ni vema
watumishi wenye utalaam katika fani mbalimbali wakatoa elimu ya kuwawezesha walengwa
kutimiza malengo yao badala ya kuwaachia Waratibu wa TASAF pekee.
Aidha,
amewataka walengwa wa TASAF kutumia vizuri ruzuku wanayoipata kujikwamua katika
lindi la umaskini ili hapo baadae waache kutegemea ruzuku ya TASAF.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kilio kikubwa cha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kilikuwa ni suala la upandishwaji wa madaraja jambo ambalo limetekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
“Mhe. Naibu Waziri tunashukuru sana kwa kututembelea, changamoto kubwa iliyokuwa ikitusumbua ni upandishwaji wa madaraja, suala ambalo limeshafanyiwa kazi, tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuliona hili na kulitekeleza.” Mhe. Ridhiwan ameongeza.
Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika
halmashauri hizo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma, kukagua
utekelezaji wa miradi ya TASAF, ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na utekelezaji
wa maelekezo ya Mhe. Rais ya upandishwaji wa madaraja kwa Watumishi wa Umma nchini.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani (hawapo
pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma mkoani humo.
Baadhi ya
Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza
nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi
yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Afisa Misitu wa
Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani, Bw. William Msemo akiwasilisha hoja ya
kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza
nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji huo wakati wa ziara yake ya kikazi yenye
lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kitongoji
cha Mwanabwito wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha (hawapo pichani) wakati wa
ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF
mkoani Pwani.
Walengwa wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa Kitongoji cha Mwanabwito, Halmashauri ya
Wilaya ya Kibaha wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi
ya TASAF mkoani Pwani.
Mbunge wa Jimbo la
Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma Wilayani Chalinze.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha
Vijijini, Mhe. Michael Mwakamo akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma na kukagua miradi ya TASAF wilayani Kibaha.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu
wa TASAF, Bw. Paul Kijazi akitoa maelezo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuhusu
mradi wa jengo la kitega uchumi la kikundi cha Wazee wa Mlandizi lililojengwa
na TASAF.
Kikundi cha Wazee wa
Mlandizi kilichonufaika na mradi wa jengo la kitega uchumi lililojengwa na
TASAF wakiwa mbele ya jengo hilo.
No comments:
Post a Comment