Na. James K. Mwanamyoto – Namtumbo
Tarehe 20 Agosti, 2020.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetakiwa kuhakikisha
wananchi wanapata haki wanazostahili popote pale wanapoenda kupata huduma
nchini, iwe ni kwenye taasisi za umma au binafsi.
Agizo hilo limetolewa wilayani Namtumbo jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati
akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, TAKUKURU inatakiwa kuwajengea wananchi imani
ya kiutendaji ili pale inapotokea wananyang’anywa haki zao na mtu au taasisi
yoyote kwa njia za rushwa, TAKUKURU ndio iwe ni kimbilio lao huku wakiwa na
imani kuwa watasaidiwa ipasavyo na taasisi hiyo.
“Nawasihi, endeleeni kuwang’ata wala rushwa na mafisadi wote ili mradi
msimuonee au kumpendelea yeyote, na endeleeni kuifanya haki ndio nguzo ya
utendaji kazi wenu wa kila siku,” Mhe. Mkuchika alihimiza.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Sabina Seja akitoa maelezo
kuhusu jengo hilo alisema, uzinduzi wa jengo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo ni
ushaidi tosha kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli imeonesha nia na dhamira ya dhati ya kukabiliana na vitendo vya
rushwa, ubadhirifu wa mali za umma nchini.
Bibi Seja, amemtibitishia Mhe. Mkuchika kuwa, Watumishi wa TAKUKURU
wilayani Namtumbo watatumia jengo la ofisi hiyo kuhakikisha wanapambana na
vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu kwa manufaa ya wananchi na maslahi ya
taifa.
Mhe. Mkuchika amezindua jengo hilo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye tangu aingie madarakani amefanya kazi
kubwa ya kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Namtumbo (hawapo pichani) kabla ya kuzindua Jengo la ofisi ya TAKUKURU la wilaya hiyo Agosti 19, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst)
Mhe. George H. Mkuchika akikata utepe kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya
ya Namtumbo, Agosti 19, 2020. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe.
Christina Mndeme na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst)
Mhe. George H. Mkuchika akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo.
Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme na Kaimu Mkurugenzi wa
TAKUKURU, Bibi Sabina Seja.
Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja akitoa
maelezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika kuhusu
jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo kabla ya Waziri huyo kulizindua
rasmi Agosti 19, 2020.
No comments:
Post a Comment