Chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania (TPSC) kimetakiwa kuhakikisha kinafanya tafiti zenye tija
zitakazoiwezesha Serikali kufanya maboresho ya utendaji kazi katika taasisi za
umma nchini, ili taasisi hizo ziweze kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa jana na
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo cha Utumishi
wa Umma yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora.
Dkt. Mwanjelwa amesisitiza
kuwa, taasisi zinazofanywa ni lazima ziendane na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi
hususani wakati huu ambao nchi imeingia katika uchumi wa kati.
“Ni
muhimu kufanya tafiti zenye tija katika kuboresha Utumishi wa Umma ili uwe na
manufaa katika maendeleo ya kichumi na taifa kwa ujumla,” Dkt. Mwanjelwa
alisisitiza.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa
amewataka waajiri katika taasisi za umma kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata
mafuzo yanayotolewa na TPSC ili
kuwaongezea ujuzi na weledi utakaowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za
Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha huduma kwa umma.
Sanjali na hilo, Dkt.
Mwanjelwa amewahimiza waajiri kuwawezesha watumishi kupata mafunzo maalum ya kuwaandaa kufanya
mitihani ya Utumishi wa Umma kulingana na kada zao ambayo ipo kwa mujibu wa
taratibu za kiutumishi.
Katika hatua nyingine Dkt.
Mwanjelwa amewakumbusha wahitimu kujilinda dhidi ya magonjwa hatarishi
yatakayoathiri afya zao na kushindwa kutumia elimu na ujuzi walioupata katika
ujenzi wa taifa.
Kwa upande wake, Mtendaji
Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika
amesema, chuo kimeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kitaaluma ili
kuhakikisha Watumishi wa Umma na wananchi wanaopata fursa ya mafunzo katika
chuo chake wanapata elimu bora na ujuzi utakaowawezesha kutoa mchango katika
maendeleo ya taifa.
Kuhusu idadi ya wahitimu,
Dkt. Shindika amesema, jumla ya wanachuo 1,917 kutoka katika kampasi sita za
Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Mbeya, Singida na Tanga wamehitimu katika
Mahafali ya 32 ya Chuo cha Utumishi wa Umma
kwa mwaka 2020 yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa, akiongoza maandamano ya Wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 32 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora. Kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Charles Msonde.
Naibu Waziri , Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa akimtunuku cheti mmoja wa wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo hicho yaliyofanyika jana katika Kampasi ya Tabora.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa akiimba wimbo pamoja na wanakwaya wa Chuo cha Utumishi wa Umma wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo hicho mjini Tabora yaliyofanyika jana katika Kampasi ya Tabora.
No comments:
Post a Comment