Na. James K.
Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 01 Julai,
2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezindua huduma mpya ya kibenki nchini ya Hekima Banking Tabasamu la Kustaafu inayotolewa na Benki ya Stanbic ili kutatua changamoto zinazowakabili wastaafu ikiwemo ya kutapeliwa mafao yao.
Waziri Jenista amesema, ana imani kuwa, hakuna mstaafu atakayeangukia kwenye mikono ya wadhalimu iwapo atapata elimu inayotolewa na Benki ya Stanbic kuhusu Huduma ya Hekima Banking almaarufu kama Tabasamu la Kustaafu.
“Baada ya kupata elimu hii ya Hekima Banking, kila mstaafu atakuwa ametengenezewa utaratibu, miundombinu na mfumo mzuri wa kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi ambao utamuwezesha kuishi maisha mazuri yenye tabasamu baada ya kustaafu,” Mhe. Jenista amefafanua.
Akizungumzia wimbi la utapeli wanaofanyiwa wastaafu, Mhe. Jenista amesema, akiwa ndiye waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma, anatoa onyo kwa matapeli wote ambao wamekuwa wakijiandaa kwa kuweka mikakati ovu ya kuwatapeli watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu na waliostaafu.
Kuhusu ubunifu wa Benki ya Stanbic kuanzisha huduma ya Hekima Banking kwa ajili ya kutatua changamoto za wastaafu, Mhe. Jenista ameishukuru na kuipongeza benki hiyo na kuziomba taasisi nyingine za kifedha kubuni huduma za kuwasaidia wastaafu kuwekeza mafao yao ili wawe na maisha mazuri yenye tabasamu la kudumu baada ya kustaafu.
“Kama taasisi zote za kifedha zitasimama imara na kufanya jambo zuri kama hili la Benki ya Stanbic la kuwaandalia wastaafu huduma nzuri ya kuwa na uwekezaji sahihi kupitia mafao yao, nina imani kuwa, wastaafu wote watawezeshwa kuwa na maisha mazuri yenye tabasamu la uhakika baada ya kustaafu,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha, ameongeza kuwa, taasisi za kifedha zikibuni huduma za kibenki kwa ajili ya kuwawezesha wastaafu kuwa na uwekezaji sahihi wa mafao yao, zitasaidia sana wastaafu kumudu gharama za maisha zikiwemo za matibabu, chakula na kusomesha kwa wastaafu ambao bado wanaendelea kusomesha watoto wao.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa Rejareja cha Benki ya Stanbic, Bw. Omari Mtiga amesema, benki yao inayo furaha kubwa kuleta huduma ya Hekima Banking yenye kibwagizo cha tabasamu la kustaafu kwa wateja wao na watanzania kwa ujumla ili huduma hiyo iwanufaishe wastaafu wote nchini.
Bw. Mtiga amesema kuwa, Benki ya Stanbic imeanzisha huduma hiyo ya Hekima Banking maalumu kwa wastaafu baada ya kufanya utafiti wa zaidi ya miaka miwili uliolenga kuangalia ni nini watumishi wanaotarajia kustaafu na waliostaafu wanahitaji katika eneo la uwekezaji kupitia mafao, hivyo wao kama wataalamu wamekuja na huduma hiyo ambayo ni suhuhisho la changamoto zinazowakabili wastaafu wengi nchini.
Benki ya
Stanbic imebuni na kuja na Huduma ya Hekima Banking maalumu kwa wastaafu nchini,
ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuweka mazingira bora
ya kuwawezesha wastaafu kuishi maisha mazuri baada ya kumaliza jukumu la
kulitumikia taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wanaotarajia kustaafu, wastaafu
na watendaji wa Benki ya Stanbic kabla ya kuzindua huduma mpya ya kibenki ya Hekima
Banking Tabasamu la Kustaafu inayotolewa na Benki ya Stanbic kwa ajili ya
kuwawezesha wastaafu kuwekeza ili kuwa na maisha mazuri baada ya kustaafu.
Baadhi
ya watumishi wanaotarajia kustaafu, wastaafu na watendaji wa Benki ya Stanbic
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kabla ya waziri huyo kuzindua
huduma mpya ya kibenki ya Hekima Banking Tabasamu la Kustaafu inayotolewa na
Benki ya Stanbic kwa ajili ya kuwawezesha wastaafu kuwekeza ili kuwa na maisha
mazuri baada ya kustaafu.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa Rejareja cha Benki
ya Stanbic, Bw. Omari Mtiga akieleza lengo la benki yake kuanzisha huduma ya
Hekima Banking yenye kibwagizo cha tabasamu la kustaafu, kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua rasmi huduma hiyo kwa wastaafu.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akikata utepe kuzindua huduma mpya ya kibenki ya Hekima Banking
Tabasamu la Kustaafu inayotolewa na Benki ya Stanbic kwa ajili ya kuwawezesha
wastaafu kuwekeza ili kuwa na maisha mazuri baada ya kustaafu.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wanaotarajia kustaafu
na wastaafu, mara baada ya waziri huyo kuzindua huduma mpya ya kibenki ya
Hekima Banking Tabasamu la Kustaafu inayotolewa na Benki ya Stanbic kwa ajili
ya kuwawezesha wastaafu hao kuwekeza ili kuwa na maisha mazuri baada ya
kustaafu.
No comments:
Post a Comment