Thursday, July 7, 2022

MHE. JENISTA AWAELEKEZA WAAJIRI SERIKALINI KUFANYA UFUATILIAJI WA MASUALA YA KIUTUMISHI BADALA YA KUWAACHA WATUMISHI WENYEWE KUFUATILIA

Na. James K. Mwanamyoto-Songea

Tarehe 07 Julai, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka Waajiri Serikalini kufanya ufuatiliaji wa changamoto za masuala ya kiutumishi zinazowakabili watumishi wa umma ambazo zimeshindikana kutatuliwa katika maeneo yao ya kazi badala ya kuwaacha wahusika kufuatilia wenyewe Makao Makuu ya Nchi Dodoma. 

Mhe. Jenista amesema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma, Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma mkoani humo. 

Mhe. Jenista amesema watumishi wote wenye changamoto ambazo haziwezi kutatuliwa na waajiri wao ni wajibu wa Waajiri na Maafisa Utumishi kufanya ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Ofisi yake kwa ajili ya kupata ushauri na maelekezo ya namna ya kutatua changamoto hizo. 

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, sio lazima kwa Maafisa Utumishi kusafiri kwa ajili ya kushughulikia changamoto za watumishi kwani kwa sasa Serikali imeboresha mifumo ya mawasiliano ambapo Afisa Utumishi anaweza kuwasiliana na Ofisi yake au taasisi nyingine ya umma kwa ajili ya kutatua changamoto husika. 

“Sasa hivi zipo njia nyingi za kidijitali zilizoanzishwa na Serikali ambazo zinawawezesha Maafisa Utumishi kuwasiliana pasipo kusafiri, kwa mfano, Ofisi yangu ina kituo cha huduma kwa mteja (call center), e-mrejesho na Sema na Waziri wa UTUMISHI, njia ambazo wanaweza kuzitumia katika utatuzi wa changamoto za kiutumishi.” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea malalamiko ya kiutumishi ya Afisa Elimu Sayansikimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Sr. Chrisma Ngonyani ambaye hajalipwa malimbikizo ya mishahara ya miezi tisa kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu za malipo ya mshahara wa mwezi Juni, 2011 zitakazosaidia kuwezesha malipo ya madai yake. 

Kufuatia malalamiko ya mtumishi huyo, Waziri Jenista amemuelekeza Mwajiri na Afisa Utumishi wake kufuatilia suala hilo Wizara ya Fedha ili mchakato wa kushughulikia madai hayo uendelee na kuongeza kuwa iwapo watahitaji msaada kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, watendaji wake wako tayari kutoa ushirikiano. 

Mhe. Jenista amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkoa wa Ruvuma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa mkoa huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Afisa Elimu Sayansikimu, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Sr. Chrisma Ngonyani, akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.


 

No comments:

Post a Comment