Tuesday, December 12, 2023

WATUMISHI WA UMMA KUJAZA KAZI WANAZOFANYA KATIKA MFUMO MAHALI POPOTE

 Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi- Dodoma

Tarehe 12 Desemba, 2023

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais- UTUMISHI ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Utumishi wa Umma kwa kuhimiza uwajibikaji wa hiari wa mtumishi kwa kujaza kazi anazofanya kila siku katika mfumo mahali popote ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa umma.

Ameyasema hayo leo tarehe 12 Desemba, 2023 wakati wa kufungua mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS na PIPMIS) na Mfumo Maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini (HR Assesment) kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Bi. Felista amefafanua kuwa mfumo wa PEPMIS utawezesha viongozi kusimamia utendaji kazi wa watumishi bila upendeleo na utaongeza ufanisi, PIPMIS itawezesha kupima utendaji kazi wa Taasisi za Umma  na HR Assesment itawezesha kufanya Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini na kuitumia ipasavyo.

Aidha, Bi. Shuli ameongeza kuwa hali ya mafunzo kwa Mkoa wa Dodoma inaendelea vizuri na anaamini yatakamilika kama ilivyopangwa kwa kuwa pande zote zinazohusika na mafunzo zinatoa ushirikiano mkubwa kwa wakati.

“Wawezeshaji wote wako vizuri na watumishi kutoka katika Wizara na Taasisi zote wanaitikia wito na wanakuja na kompyuta ambazo ni kitendea kazi muhimu sana katika mafunzo haya” amesema Bi.Felista.

Vilevile, amesema mfumo wa PEPMIS umekuja kuwa mbadala wa OPRAS ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayowezesha viongozi na watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakati na mahali popote.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Fedha Bw. Renatus Msagira amesema watumishi wako tayari kujifunza na kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi kwa maendeleo ya taifa.

“Tuko tayari na hatutakuwa kikwazo katika utekelezaji wa jitihada hizi muhimu za Serikali ambazo lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati” amesisitiza Bw. Msagira.

Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment yanaendeshwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mikoa yote Tanzania Bara na yatahitimishwa Desemba 31,2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Fedha wakati akifungua Mafunzo ya Mifumo hiyo katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Fedha wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli (hayupo pichani) wakati akifungua Mafunzo ya Mifumo hiyo jijini Dodoma.


Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utawala, Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Nyasinde Mukono (Aliyesimama) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA. Habibu Suluo (Wa kwanza kulia) wakati wa Mafunzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) kwa Menejimenti ya LATRA yaliyofanyika katika ukumbi mdogo wa Bunge jijini Dodoma.


Menejimenti ya LATRA ikiendelea na mafuzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendaji kazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) yanayoendeshwa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI jijini Dodoma.


Baadhi ya Viongozi wa LATRA wakifanya mafunzo kwa vitendo ya Mfumo wa Upimaji na Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) yanayotolewa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI jijini Dodoma.



Afisa Utumishi Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Judith Abdallah akiwaelekeza washiriki wa Mafunzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) kutoka TANESCO, REA na EWURA jijini Dodoma.


Washiriki kutoka TANESCO, REA na EWURA wakiwa kwenye mafunzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) yanayotolewa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention jijini Dodoma.

 





 



No comments:

Post a Comment