Na. James K.
Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 02 Aprili,
2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameilekeza Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kufanya ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma zinazotoa huduma moja kwa moja kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe.
Jenista ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na
Waandishi wa Habari kuhusiana na uhitimishaji
wa zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha
2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Mhe.
Jenista amesema, upo umuhimu mkubwa wa kufanya ukaguzi kwenye taasisi zinazotoa
huduma muhimu kwa wananchi kama za afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na uvuvi
ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.
Akizitaja
faida za ukaguzi wa rasilimaliwatu, Waziri Jenista amesema, una faida kubwa kwa
Serikali, Waajiri, Watumishi wa Umma na Watanzania kwa ujumla ambao ndio
walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi zake.
Ameongoza
kuwa, unazisaidia pia taasisi zilizokaguliwa kurekebisha kasoro za kiutendaji
ambazo zimebainishwa wakati wa ukaguzi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa
wananchi.
Pia
amesema ukaguzi huo unaiwezesha Serikali kufahamu hali ya utendaji kazi iliyopo
katika taasisi za umma na kuziwezesha mamlaka husika kufanya maamuzi
yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa taasisi zote za umma.
Sanjali
na hayo, Waziri Jenista amesema ukaguzi huo unaipa fursa Tume ya Utumishi wa
Umma kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya namna bora ya kuboresha Sera, Sheria,
Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo ili iwe na tija kwa
umma na taifa kwa ujumla.
Kuhusiana
na migogoro ya kiutendaji inayojitokeza kwenye baadhi ya taasisi, Mhe. Jenista
amesema taasisi hizo zikitekeleza maelekezo ya Tume baada ya kufanyiwa ukaguzi
zitaepusha migogoro kwa kiasi kikubwa.
Tume
ya Utumishi wa Umma imekamilisha zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu kwenye
Taasisi za Umma 110, hivyo taarifa ya ukaguzi huo inaandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa
kwenye mamlaka husika kwa hatua stahiki.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa
rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa
na Tume ya Utumishi wa Umma.
Baadhi
ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma na Waandishi wa Habari wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa
zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022
lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew
Kirama akitoa neno la
utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Waandishi
wa Habari jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa
rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa
na Tume ya Utumishi wa Umma.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari alipokuwa akielezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa
rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa
na Tume ya Utumishi wa Umma. Kulia kwake ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma,
Bw. Mathew Kirama.
No comments:
Post a Comment