Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 28 Aprili, 2022
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama amezitaka Taasisi zote za Umma nchini kupata kibali cha Mamlaka
ya Serikali Mtandao kabla ya kutekeleza Miradi ya TEHAMA ili kuondoa changamoto
ya kutowasiliana na kubadilishana taarifa kwa mifumo hiyo na hatimaye kupoteza
mapato ya Serikali.
Akifungua
kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini jijini Dodoma, Mhe.
Jenista amesema iwapo utekelezaji wa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA
utawianishwa na kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa ndani ya taasisi za umma na
baina ya taasisi za umma, utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao utakuwa ni
kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yanayokusudiwa kwa taifa.
Mhe.
Jenista amesema Serikali ilianzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao kupitia Sheria
ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, na kuipa jukumu la kusimamia,
kuratibu na kuendeleza utekelezaji wa Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia
uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika
Taasisi za Umma.
Amesema
pamoja na uanzishwaji wa Mamlaka hiyo bado kumekuwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo mifumo isiyowasiliana au kubadilishana taarifa ndani ya taasisi, na
kati ya taasisi na taasisi, urudufu wa mifumo miongoni mwa Taasisi za Serikali
yenye viwango na gharama tofauti zisizo na uhalisia, huduma za Serikali Mtandao
kutowafikia wananchi wote hasa wa vijijini na kuongezeka kwa matishio ya
usalama wa taarifa katika mifumo na Miundombinu ya TEHAMA.
Kutokana
na changamoto hiyo, Mhe. Jenista, ameiagiza Mamlaka ya Serikali mtandao
kuhakikisha mifumo inayofanana inaunganishwa na ile isiyofanana inaboreshwa na
kubadilishana taarifa ifikapo tarehe 30 Septemba, 2022.
Aidha,
Mhe. Jenista amewataka wataalam hao kujenga mifumo ya utoaji huduma ambayo ni
rafiki kwa watumiaji ili kila mwananchi aweze kunufaika na huduma zinazotolewa
na Serikali kwani mifumo hiyo inajengwa kwa ajili ya kuwahudumia wao.
Mhe.
Jenista amesema, Serikali imeamua Utumishi wa Umma kuwa wa kidijitali katika
maeneo yote ya utendaji kazi hivyo, ushirikiano mkubwa unahitajika kutoka kwa
Wataalam wa TEHAMA kwani wao ndio wanaoweza kusaidia lengo hilo kufikiwa.
“Kwa
niaba ya Serikali niwaombe Wataalam wa TEHAMA mvae uzalendo, muwajibike kwa
hiari bila kushurutishwa, ili muweze kutuvusha na kuwa na Serikali ya
kidijitali kwa utoaji wa huduma bora kwa umma.” Mhe. Jenista amesisitiza.
Akizunguzia
umuhimu wa TEHAMA Serikalini, Mhe. Jenista amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo
ya mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26)
na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 kwa pamoja zinatambua
nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya Taifa na hivyo kusisitiza haja ya
ongezeko la matumizi yake katika utendaji wa shughuli za Serikali na utoaji
huduma kwa Umma.
Mhe.
Jenista amewataka wataalam hao wa TEHAMA kujifunza kwa nchi za Malaysia,
Singapore na Korea ya Kusini walivyopiga hatua katika maendeleo ya TEHAMA na
kuongeza kuwa kabla yao, Tanzania ilipiga hatua katika suala la TEAHAMA lakini
leo wao wako mbele yetu.
Mhe.
Jenista ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kuandaa kikao kazi hicho
muhimu ambacho pamoja na mambo mengine kinawakumbusha Wataalam wa TEHAMA
umuhimu wa uzingatiaji wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019 na
kuelekeza kufanyika kwa kikao kazi kama hicho kila mwaka ambacho pia
kitawatambua wanaofanya vizuri katika kuzingatia Sheria ya Serikali Mtandao na
wanaosizingatia sheria watatajwa lengo likiwa ni kutaka wote wazingatie sheria.
Kikao
kazi hicho ambacho ni cha pili kufanyika tangu kutungwa kwa Sheria ya Serikali
Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, kimeshirikisha Wakuu wa Idara na Vitengo vya
TEHAMA 486 kutoka kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Idara zinazojitegemea,
Mamlaka, Wakala, Mikoa, Majiji, Manispaa
na Halmashauri za Wilaya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Idara na
Vitengo vya TEHAMA Serikalini jijini Dodoma.
Sehemu ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini
wakimsikiliza Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Idara na
Vitengo vya TEHAMA Serikalini jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Hassan Kitenge akitoa
neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Idara na Vitengo
vya TEHAMA Serikalini jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA),
Mhandisi Benedict Ndomba akielezea lengo la kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA
Serikalini kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kabla ya
Mhe. Jenista kufungua kikao kazi hicho jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Idara na
Vitengo vya TEHAMA Serikalini jijini Dodoma. Wa kwanza kulia kwake ni Kaimu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Hassan Kitenge na wa kwanza kushoto kwake ni
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba.
Mkurugenzi wa TEHAMA, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango akitoa neno la shukrani
kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya Waziri Jenista kufungua kikao
kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini jijini
Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara na
Vitengo vya TEHAMA Serikalini mara baada ya kufungua kikao kazi cha Wakuu wa
Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini jijini Dodoma. Wa kwanza kulia kwake ni Kaimu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Hassan Kitenge na wa kwanza kushoto kwake ni
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwasili kwenye ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, habari
na mawasiliano Chuo Kikuuu Dodoma
kufungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini
jijini Dodoma. Wa kwanza
kulia kwake ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Hassan Kitenge na
wa kwanza kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
Mhandisi Benedict Ndomba.
No comments:
Post a Comment