Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisoma wasifu wa Hayati
Benjamin William Mkapa wakati wa Ibada ya mazishi ya Rais Mstaafu huyo wa Awamu
ya Tatu yaliyofanyika kijiji cha Lupaso mkoani Mtwara, amesema hayati Benjamin
William Mkapa aliutumikia umma katika nyadhifa mbalimbali hivyo atakumbukwa na Watanzania
wote kwa utumishi wake uliotukuka.
Dkt. Ndumbaro alifafanua
kuwa, Hayati Benjamin William Mkapa alianza kazi rasmi Serikalini kama Afisa
Tawala katika Wilaya ya Dodoma, Mkoani Dodoma mnamo Mwezi Aprili, 1962 kabla ya
kujiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Diplomasia katika Chuo Kikuu cha
Columbia nchini Marekani.
Alisema, mara baada ya
kuhitimu shahada hiyo ya Uzamili nchini Marekani, Hayati Mkapa alirejea nchini
na kufanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwenye Dawati la Afrika akiwa na
cheo cha Afisa wa Mambo ya Nje.
Aliainisha kuwa, akiwa Afisa
wa Mambo ya Nje, miongoni mwa kazi alizokuwa akizifanya ni pamoja na kuchukua
muhtasari wa mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje au Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania anapokuwa na wageni.
Dkt. Ndumbaro aliongeza
kuwa, sehemu kubwa ya utumishi wa Hayati Benjamin William Mkapa Serikalini, alihudumu
kama kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ambapo mnamo Aprili, 1972 aliteuliwa
kuwa Mhariri Mtendaji wa kwanza wa Magazeti ya Serikali ya Kiingereza ya Daily
News na Sunday News.
Dkt. Ndumbaro alisema, mwaka
1974 hadi 1976 Hayati Benjamin William
Mkapa aliteuliwa kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa na mnamo mwaka 1976
aliteuliwa kuanzisha Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na kuhudumu katika
shirika hilo kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika.
Sanjali na nafasi hizo,
mwaka 1977 Hayati Benjamin William Mkapa aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje
na kufanikiwa kuiongoza Wizara hiyo kwa miaka mitatu, na mwaka 1982 alihudumu
kama Balozi wa Tanzania nchini Canada na ilipofika mwaka 1983 alihamishiwa nchini Marekani kuwa Balozi
wa Tanzania nchini humo ambako alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1984.
Kutokana na utendaji kazi
mzuri wa Hayati Benjamin William Mkapa, mnamo mwaka 1984 aliteuliwa tena kuwa
Waziri wa Mambo ya Nje na kufanikiwa kufanya kazi hiyo kwa miaka sita hadi
mwaka 1990 alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji na kuifanya
kazi hiyo hadi mwaka 1992.
Aidha, Dkt. Ndumbaro
alisema, Mwaka 1992 Hayati Benjamin William Mkapa alihudumu kama Waziri wa
Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wadhifa alioutumikia hadi mwaka 1995
alipoamua kugombea na akashinda Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisoma wasifu wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa wakati wa mazishi ya Hayati Mkapa Kijijini Lupaso mkoani Mtwara.
HAYATI MKAPA ALICHUKIA SANA RUSHWA NA UMASKINI NA KUAMUA KUANZISHA TAKUKURU, TASAF NA MKURABITA
Na Mary Mwakapenda- Masasi
Tarehe 29 Julai, 2020
Hayati Benjamin William
Mkapa wakati wa utawala wake pamoja na mambo mengine aliyoyafanya kwa manufaa ya Taifa, atakumbumbukwa
na watanzania kwa kuchukia rushwa na umaskini na hatimaye kuanzisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha
Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ambapo kwa kiwango
kikubwa TAKUKURU imesaidia kupambana na Rushwa wakati TASAF na MKURABITA zimeboresha maisha ya
wananchi wenye kipato cha chini.
Hayo yamesemwa jana na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma
Mkuchika (Mb) kijijini Lupaso-Masasi alipokuwa akikagua maandalizi ya sehemu ambayo
mwili wa Hayati Mkapa utapumzishwa.
Akifafanua kwa undani sababu
za Hayati Mkapa kuanzisha Taasisi hizo, Mhe. Mkuchika amesema kuwa, alichukia sana
rushwa, hivyo alimteua Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba kufanya utafiti ili kujua
sababu za rushwa, mianya ya rushwa na nini kifanyike kuzuia rushwa nchini na matokeo
ya utafiti huo yakawa ni chachu ya kuanzisha na kuimarishwa kwa TAKUKURU.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa,
Hayati Mkapa alichukia sana umasikini na aligundua kwamba Watanzania wengi waliishi
maisha duni ya mlo mmoja kwa siku, hivyo aliwasisitiza wananchi kupambana na umaskini
na kwa huruma yake alianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kuzisaidia
kaya maskini, Mfuko ambao uliendelezwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye hivi karibuni alizindua Sehemu ya Pili
ya Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Aidha, amesema, Hayati Mkapa alianzisha MKURABITA ili wananchi wapate Hati
za Hatimiliki za Kimila zinazotolewa kwa Mujibu wa Sheria Na. 5 ya Ardhi ya
Vijiji ya Mwaka 1999 ambazo zinawawezesha kujipatia mikopo kwenye taasisi za kifedha
na kujikwamua kiuchumi.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,
Hayati Benjamin William Mkapa alifariki dunia tarehe 23/07/2020 na anazikwa leo
Kijijini kwake Lupaso-Masasi, Mkoani Mtwara.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George
Huruma Mkuchika (Mb) akisaini Kitabu cha Maombolezo Kijijini Lupaso - Masasi
nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini William Mkapa
aliyefariki dunia tarehe 23/7/2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George
Huruma Mkuchika (Mb) akiwaeleza Waandishi wa Habari Kijijini Lupaso - Masasi kuhusu
jitihada alizozifanya Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa katika kupambana na rushwa
na umaskini nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George
Huruma Mkuchika akimsikiliza Bw. Dunstan Mkapa ambaye ni Mdogo wa Rais Mstaafu
wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini William Mkapa, wakati akizungumza nae Kijijini
Lupaso – Masasi. Kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Alphayo
Kidata.
No comments:
Post a Comment