Na. James K. Mwanamyoto - Mwanza
Tarehe 05 Oktoba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watendaji Wakuu wa Taasisi za
Umma zilizoko Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanawasilisha nyaraka zenye umuhimu kitaifa
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Na.
3 ya Mwaka 2002.
Mhe. Mchengerwa ametoa
maelekezo hayo wakati akizindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo jijini
Mwanza.
Mhe. Mchengerwa amesema
waajiri wanao wajibu wa kuhamishia kumbukumbu zote muhimu katika kituo hicho ili
ziweze kutunzwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya matumizi
ya sasa na vizazi vijavyo.
Mhe. Mchengerwa ameongeza
kuwa, miundombinu ya kituo hicho cha Kumbumbuku alichokizindua ni ya kisasa inayowezesha
kutunza kumbukumbu za nyaraka kidijitali.
“Kituo hiki kina
uwezo mkubwa wa kuhifadhi majalada, hivyo kitawezesha taasisi zote za umma kuokoa
zaidi ya mita za mraba 16,600 za ofisi zao ambazo zingetumika kuhifadhi majalada
hayo,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Akizungumzia lengo la
uanzishwaji wa kituo hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Naibu Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Francis
Michael amesema ujenzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa juhudi za Serikali za kuhakikisha
kuwa taarifa, kumbukumbu na nyaraka zinazalishwa katika mifumo iliyokubalika kwa
mujibu wa sheria na miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kutuzwa katika mazingira bora na salama kwa manufaa ya
taifa.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi
amesema Kituo hicho cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kitaunganishwa na mifumo ya Serikali
Mtandao, hivyo nyaraka zinazokusanywa na kuhifadhiwa zitawekwa katika mifumo ya kidijitali.
Bw. Msiangi ameongeza
kuwa, nyaraka zinazozalishwa na taasisi za umma katika mifumo ya kidijitali zitapokelewa
moja kwa moja kidijitali kutoka katika taasisi za umma.
Naye, Mkurugenzi Mstaafu
wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa aliyetafuta kiwanja mwaka 1982
ambacho Kituo hicho kimejengwa, Mzee Silvin Mongella ameishukuru Serikali kwa kuona
umuhimu wa kutoa fedha za kujenga kituo cha kuhifadhi kumbukumbu Kanda ya Ziwa.
Mzee Mongella amewahimiza
watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kufanya kazi kwa bidii kwani
hivisasa nyaraka ni nyingi na zinahitaji kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo
na kuongeza kuwa, wasipotekeleza wajibu wao kikamilifu watawanyima haki Watanzania
kujua utamaduni wao na historia yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
amezindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa Mwanza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kituo ambacho kinatoa huduma
katika Mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga,
Simiyu na Kagera.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi na wageni waalikwa kabla ya
kuzindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
Sehemu
ya Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wakimsikiliza Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuzindua
Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akielezea lengo la Serikali la kujenga Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo jijini Mwanza.
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi,
akitoa maelezo ya awali kuhusu Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo
jijini Mwanza.
Mkurugenzi
Mstaafu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ambaye pia ni mwasisi wa
Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa, Mzee Silvin Mongella akielezea historia ya
upatikanaji wa kiwanja ambacho Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kimejengwa.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akikata utepe kuzindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa
jijini Mwanza.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akisoma ujumbe wa kibao cha uzinduzi wa Kituo cha Kumbukumbu
Kanda ya Ziwa mara baada ya kuzindua kituo hicho jijini Mwanza. Pembeni yake ni
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe.
Amina Makilagi
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiangalia mchoro wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa
baada ya kuzindua kituo hicho jijini Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiangalia moja ya nyaraka zilizoko katika Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa baada ya kuzindua kituo hicho jijini Mwanza.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa baada ya Mhe. Mchengerwa kuzindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda
ya Ziwa jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment