Na. Veronica Mwafisi-ARUSHA
Tarehe 17 Oktoba, 2021
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Waajiri katika
Taasisi za Umma kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwapatia haki
kwa wakati Watumishi wa Umma wanaotekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwajengea
morali ya utendaji kazi.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo
jijini Arusha kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo cha Uhasibu Arusha
(IAA) akiwa kwenye ziara yake ya kikazi, yenye lengo la kusikiliza na
kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi hao wa umma.
Dkt. Ndumbaro amesema, suala la
uzingatiaji wa haki za Watumishi wa Umma limepewa kipaumbele na Serikali ya
Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo viongozi katika
Taasisi za Umma wanapaswa kutenda haki kwa watumishi walio chini yao ili watumishi
hao waweze kufanya kazi kwa moyo na uzalendo.
Sanjari na hilo, Dkt. Ndumbaro
amehimiza suala la uadilifu katika Utumishi wa Umma ambalo limepewa msisitizo
na Serikali ya Awamu ya Sita hivyo amewataka viongozi katika taasisi zote za
umma kuwa mfano wa kuigwa kwa uadilifu.
“Watumishi wa Umma tunapaswa
kuwa waadilifu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo
katika Utumishi wa Umma,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amehimiza
uwajibikaji katika Utumishi wa Umma kwa kuwataka viongozi na Watumishi wa Umma
kuwajibika ipasavyo kwa Serikali iliyopo madarakani kwa wananchi wanaofuata
huduma katika Taasisi za Umma.
“Serikali inawahimiza waajiri
kuhakikisha Watumishi wa Umma wanafanya kazi kwa bidii, juhudi, maarifa na watambue
mchango wa watumishi wanaofanya kazi kwa bidii,” Dkt. Ndumbaro amefafanua.
Kuhusiana na watumishi
wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao, Dkt. Ndumbaro amewataka waajiri
kuwachukulia hatua stahiki ili wabadilike na kuendana na Kaulimbiu ya Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.
“Tuwachukulie hatua watumishi
wote wanaobainika kutofanya kazi kwa bidii, tuwarekebishe kwa maneno au
kuwaandikia barua, hivyo wasionewe haya kwani wataharibu taswira nzuri ya
Utumishi wa Umma,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amehitimisha ziara yake
ya kikazi ya siku moja jijini Arusha, iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na
kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma wa Chuo cha Ufundi
Arusha (ATC) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na
watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Uhasibu Arusha kuhusu masuala
ya kiutumishi wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Arusha yenye
lengo la kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi hao.
Baadhi ya Watumishi wa Chuo
cha Ufundi Arusha wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyekaa katikati meza kuu) wakati wa
ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo, iliyolenga kusikiliza na kutatua kero
zinazowakabili watumishi wa chuo hicho.
Mtumishi wa Chuo cha Uhasibu
Arusha, Bi. Anna Nyambo akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
(hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo yenye lengo la kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha.
Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha,
Dkt. Musa Chacha (aliyenyoosha kidole) akimuonyesha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyevaa kofia
nyekundu) mchoro wa jengo la kituo cha afya katika Chuo cha Ufundi Arusha
wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu
huyo iliyokuwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi wa chuo hicho.
Afisa Utumishi wa Ofisi ya
Rais - UTUMISHI, Bi. Salama Mohamed (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo kwa baadhi
ya Watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha waliowasilisha changamoto za masuala ya
kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) iliyolenga kutatua
changamoto za watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Uhasibu Arusha.
Kushoto kwake ni Afisa Utumishi, wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Ally Ngowo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati mstali wa
mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha mara
baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Arusha iliyokuwa
na lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa chuo hicho. Kulia
kwake ni Mkuu wa Chuo hicho cha Ufundi Arusha, Dkt. Musa Chacha.
No comments:
Post a Comment