Na.
James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 20 Oktoba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi
ya utoaji haki ili kumuwezesha kila Mtanzania kupata huduma bora zinazotolewa
na Taasisi za Umma nchini.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo jana usiku jijini Dar es
Salaam, wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Kassim Majaliwa kwenye Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume
Muhammad S. A. W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa amesema, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia
Suluhu Hassan anasisitiza sana viongozi na watendaji katika taasisi zote za
umma kutenda haki ili wananchi wapate huduma stahiki.
“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais
kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninawahakikishia kuwa, Serikali ya
Awamu ya Sita itajikita katika misingi ya haki ili kila mmoja wetu apate haki,”
Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora ambayo anaiongoza imeendelea na itaendelea kuwasisitiza
viongozi na watumishi wote wa umma katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanatenda
haki ili wananchi wafurahie huduma zitolewazo na Serikali kupitia taasisi zake.
Mhe. Mchengerwa amewaomba Watanzania wote kila mmoja kwa
imani yake kumuombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuwa na afya njema
itakayomuwezesha kutimiza ndoto yake ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewata Watanzania wote kuilinda
amani kwani Mtume Muhammad S. A. W aliwaasa binadamu wote bila kujali itikadi
zao kiimani, kulinda amani na ndio maana Mhe. Rais Samia Suluhu mara kwa mara
amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza Watanzania wote kuilinda amani iliyopo.
“Amani ni lazima ianzie miongoni mwetu, ni lazima ianzie
kwenye familia zetu, tulizungumze neno amani kwenye familia zetu na kwenye
jamii yetu, na tukumbushane kuwa Tanzania ni yetu sote hivyo, tunao wajibu wa
kuilinda amani tuliyonayo,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa amewahimiza Watanzania
kuwa na mshikamano na kuthaminiana ili taifa liweze kupiga hatua haraka katika
maendeleo.
Waziri Mchengerwa amesema, kumthamini mwanadamu mwenzio
ni agizo la Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad S. A. W, hivyo Watanzania
hatuna budi kuthaminiana kwani ni agizo la Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi.
Kuhusiana na janga la COVID 19, Mhe. Mchengerwa amesema
kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwasisitiza watanzania kupata
chanjo ili kujikinga na janga hilo, hivyo amewaomba waumini wa dini zote
kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kupata chajo ya UVIKO 19 ili taifa liendelee kuwa na
wananchi wenye afya bora ambao watashiriki vema katika shughuli mbalimbali za
maendeleo.
Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi kwa niaba ya
waandaaji wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S. A. W,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara Mhe. Suleiman A.
Saddiq amesema, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ana nia njema na
taifa lake.
Ameongeza kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ana mipango
madhubuti ya kuinua uchumi wa taifa letu ili wananchi wapate ajira, huduma
nzuri za matibabu, shule na kujenga miundombinu itakayoliwezesha taifa kupiga
hatua katika maendeleo na ndio maana anajenga mahusiano na wadau wa maendeleo
duniani.
Sherehe hiyo ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika tarehe 19 Oktoba, 2021 iliandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na waumini wa dini ya
kiislam wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W
iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.
Waumini wa dini ya kiislam wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa
Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na
Biashara Mhe. Suleiman A. Saddiq akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Mchengerwa
kwa niaba ya waandaaji wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume
Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki dua ya kumuombea Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa
Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiongoza zoezi la kukata keki
katika Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa ajili ya
Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akilishwa keki na Mkurugenzi
Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi,
iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimlisha keki Mkurugenzi
Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi,
iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.
No comments:
Post a Comment