Friday, October 8, 2021

WAZIRI MCHENGERWA AWAASA WATUMISHI BUTIAMA KUMUENZI BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE KWA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA UZALENDO


Na. James K. Mwanamyoto-Mara

Tarehe 08 Oktoba, 2021 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kwa kuzingatia misingi ya uzalendo ambayo iliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya ustawi wa taifa letu.

Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mhe. Mchengerwa amesema, Butiama ndiko Baba wa Taifa alianza kusimika misingi ya uzalendo, ujamaa na kujitegemea na hata misingi ya kazi ndiko ilikoanzia na baadae kuenea nchi nzima, hivyo Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama wakati wa utekelezaji wa majukumu yao hawana budi kufuata misingi aliyoiacha.

 “Wilaya hii ya Butiama ina historia kubwa kwani ndiyo sehemu aliyozaliwa Baba wa Taifa ambaye wakati wa uhai wake alitufundisha misingi ya Utawala Bora na kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo, hivyo Wilaya hii inatakiwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa kiutendaji na Wilaya nyingine pamoja na taasisi zote za umma,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kama ilivyokuwa kwa Serikali nyingine zilizopita amekuwa akiishi kwa vitendo misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa na ndio maana akiwa ndiye mwenye dhamana ya kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora anawataka Watumishi wa Umma nchini kuendelea kuiishi misingi hiyo inayohimiza bidii ya kazi na uadilifu katika usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo. 

“Mhe. Rais Samia amekuwa akiishi misingi aliyoiacha Baba wa Taifa na ndio maana ameendelea kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoachwa na watangulizi wake na kuanzisha miradi mingine kwa maslahi ya taifa, hivyo hatuna budi kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa katika kutekeleza miradi yote ya kimkakati.

Akizungumzia ushirikiano kiutendaji, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa ushirikiano na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma ambayo Baba wa Taifa alikuwa ni muumini katika kutekeleza.

Mhe. Mchengerwa amekemea mienendo mibaya ya baadhi ya watumishi wa umma wa Butihama ambao ni walevi na watoro kazini.

“Tabia za ulevi uliopindukia, utoro kazini na tabia nyingine ambazo sio nzuri hazitakiwi katika Utumishi wa Umma, mjirekebishe ili Wilaya hii iwe mfano wa kuigwa na Wilaya nyingine na kuongeza kuwa, Serikali haiko tayari kufanya kazi na watumishi wasio waadilifu,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Mhe. Mchengerwa amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma. 

 

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Moses Kaegele akimtambulisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa Watendaji na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama alipowasili katika Halmashauri hiyo kwa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama alipowasili katika Halmashauri hiyo kwa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa kikao kwenye kikao kazi na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama alipowasili katika Halmashauri hiyo kwa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.


Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Moses Kaegele akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri hiyo.


 

No comments:

Post a Comment